TIMU ya Kijitonyama Veterans, kesho (Jumapili) itacheza mchezo maalum dhidi ya timu inayoundwa na wanamuziki wa bendi ya African Stars ‘ Twanga Pepeta’ kwenye uwanja wa Leaders Club.
Nahodha wa Twanga FC, Kalala Junior alisema kuwa mchezo huo ni maalum kwa wachezaji wake na mashabiki wa bendi hiyo baada ya kukaribisha mwaka 2013 kwa kishindo. Kalala alisema kuwa awali mchezo huo ulipangwa kuanza saa 4.00 asubuhi, waliamua kubadili muda kutokana na majukumu yao ya kazi na sasa utaanza saa 6.00 mchana.
Alisema kuwa wamechagua kucheza na timu ya Kijitonyama Veterans kutokana na umakini na heshima ya timu hiyo ambao pia inaundwa na wachezaji ambao ni wadau wakubwa wa bendi yao.
“Tumejiandaa vizuri na tunatarajia kuwa na mchezo mzuri, wachezaji na morali ya hali ya juu na lengo lao ni kufungua mwaka kwa kishindo,” alisema Kalala. Mratibu wa timu ya Kijitonyama Veterans, Majuto Omary alisema kuwa wanatarajia mchezo mzuri ambao ndiyo utawakutanisha kwa mara ya kwanza na timu hiyo ya Twanga FC.
Majuto alisema kuwa wachezaji wake wamefurahi kupata fursa hiyo na wameahidi kuibuka na ushindi mnono. “Tunajua kuwa Twanga FC inaundwa na wachezaji wazuri, tumejiandaa vizuri pia, hivyo mashabiki watarajie mchezo mzuri na wenye upinzani mkubwa, ustaharabu utakuwa wa hali ya juu kwani baada ya hapo, Twanga FC watakuwa na jukumu la kutuburudisha jukwaani,” alisema Majuto.
Mkurugenzi wa bendi ya Twanga Pepeta, Asha Baraka amewataka wachezaji wake na mashabiki kufika kwa wingi kuona vipaji vya soka vya wanamuziki wake na hasa baada ya kuanza mwaka kwa vishindo kwa upande wa burudani. Asha alisema kuwa baada ya mechi hiyo, bendi yake itafanya shoo kali ili kuwapa zawadi ya mwaka mpya kwa mashabiki wa Leaders Club.
No comments:
Post a Comment