

Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za
rambirambi Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa Xi Jinping kuombeleza
vifo vya zaidi ya watu 400 ambao wamepoteza maisha yao katika ajali ya boti ya
kitalii, iliyozama katika Mto wa Yangtze mwanzoni mwa wiki hii.
Meli ya kitalii ya
Eastern Star ilizama katika Mto wa Yangtze, karibu na mji wa Jianli, Jimbo la
Kati la Hubei, Jumatatu usiku ikiwa na abiria 456 waliokuwa wanafanya safari ya
kitalii ya siku 11 kutoka Nanjing kwenda Chongqing. Mpaka usiku wa jana,
Ijumaa, Juni 5,2015, miili ya watu 369 ilikwishapatikana, watu 46 walikuwa
hawajulikani walipo na 14 walikuwa wameokolewa.
Katika salamu zake za rambirambi, Rais Kikwete
amemwambia Rais Jinping: “Nimepokea kwa mshituko na masikitiko taarifa ya vifo
vya mamia ya watu waliopoteza maisha yao katika ajali ya boti ya kitalii ya
Eastern Star katika Jimbo la Hubei iliyotokea mwanzoni mwa wiki hii wakiwa katika
safari kutoka Nanjing kwenda Chongqing.”
“Kwa hakika, haya ni
maafa ya kitaifa. Kwa niaba ya Watanzania wenzangu, Serikali yangu na mimi
mwenyewe, nakutumia wewe binafsi, Serikali yako na wananchi wote wa China salamu
za dhati ya moyo wangu na naungana nanyi katika kuomboleza tukio hili la huzuni
kubwa.”
Ameongeza Rais
Kikwete katika salamu zake alizozituma usiku wa jana, Ijumaa, Juni 5, 2015:
“Tanzania ikiwa nchi rafiki na China na Watanzania wote wanaungana na wenzao wa
China kuwapa pole nyingi wote ambao wamepoteza wapendwa wao katika ajali hiyo.”
No comments:
Post a Comment