Habari za Punde

*WAPINZANI WA B BALL KITAA KUUMANA IJUMAA WIKI HII

 Mratibu wa B Ball Kitaa Karabani Karabani inayodhaminiwa na kinywaji cha Sprite akizungumza na waandishi wa habarileo jijini Dar-es-Salaam kuhusu mechi ya mpira wa kikapu utakaochezwa siku ya ijumaa Juni 5 wiki hii katika uwanja wa BBK Park. Kulia ni nahodha wa  timu ya East Zone 2 Haby Mayeye.
Michuano ya Bball Kitaa ngazi ya kanda inayodhaminiwa na kinywaji cha Srite, mwaka huu inatarajiwa kuzinduliwa jijini Dar es Salaam Ijumaa wiki hii, ambapo kutakuwa na pambano kali litakalozikutanisha timu kutoka kanda ya kwanza ya mashariki  ambayo inaundwa na wachezaji kutoka Msasani, Oysterbay na Masaki dhidi ya timu kutoka kanda ya pili ya magharibi ambayo inaundwa na wachezaji kutoka Mbezi Beach, Kunduchi naTegeta.
Pambano hilo ambalo linatarajiwa kuvuta hisia za ,maelfu ya mashabiki kutoka wilaya zote za jiji la Dar es Salaam yaani Kinondoni, Temeke na Ilala litafanyika katika uwanja wa Bball Kitaa Park,uliopo karibu na ukumbi maarufu wa Gymkhana jijini Dar es Salaam.
“Lengo kuu la mechi hii ni kuwafanya mashabiki wote wa kujumuika katika michuano hii mikubwa kabisa ya Bball Kitaa ngazi ya kanda, ambayo inatarajiwa kuanza Julai na kuzikutanisha kanda zote mbili za jiji la Dar es Salaam,” Karabani ambaye ni mratibu wa Bball Kitaa aliwaambia waandishi.
Karabani pia alizitaja kanda zingine ambazo zitashiriki katika michuano hiyo mwezi Julai kuwa, ni mabingwa watetezi Kanda ya Nne ya Mashariki inayoundwa na wachezaji kutoka Temeke na Mbagala, Kanda ya Kwanza ya Mashariki, Kanda ya Tatu ya Mashariki, Kanda ya Pili ya Magharibi, Kanda ya Tatu ya Magharibi na Kanda ya Kanda ya Nne ya Magharibi. Mshindi wa michuano hii ya nne ngazi ya kanda  atakabidhiwa kitita taslimu cha shilingi za Kitanzania milioni 5.
Kwa upande wake, Meneja bidhaa wa Coca-Cola nchini  Maurice Njowoka alisema kuwa kampuni ya Coca-Cola imejiona ni yenye heshima kubwa mara baada ya kupewa fursa ya kudhamini michuano hiyo nchini na kuahidi kuwa kampuni yake kuendelea kutoa ushirikiano wa bega kwa bega kuhakikisha kuwa mchezo huu unazidi kusonga mbele.
“Sote tunafahamu kuwa mchezo wa mpira wa kikapu ni mojaya michezo yenye mashabiki wengi sana nchini hasa kwa vijana ambao wanahitaji fursa hii adhimu ili kuendeleza vipaji vyao na kutimiza ndoto zao pia”, alisema Njowoka.  
Michuano ya Bball Kitaa ambayo kwa takribani miaka miwili sasa imekuwa ikifanyika nchini, imejikita katika kujenga misingi imara ya maisha na kuwaburudisha vijana na hivi karibuni Chama Cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (RBA), kimekuwa kikiitumia michuano hii kama moja ya njia za kupata vipaji vipya nchini.

“Nina furaha sana kuona Bball Kitaa sasa inatambuliwa na Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (RBA) na sote tunaamini kuwa ushirikiano huu utazidi kadiri siku zinavyokwenda ili kuendeleza mchezo huu hapa nchini”, Karabani alisema huku akizidi kumimina shukrani zake za dhati kwa  Sprite kwa moyo wao katika kuhakikisha Bball Kitaa inazidi kusonga mbele.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.