WALIOKUWA wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya vijana ya Helsinki Cup 2015, timu ya soka ya FC Vito Kilwa ya Kilwa mkoani Lindi, wametua jijini Dar es Salaam leo alfajiri, wakitokea jijini Helsinki nchini Finland walikokuwa wakishiriki michuano hiyo ya kila mwaka.
FC Vito Kilwa, inayomilikiwa kwa pamoja na Taasisi zisizo za kiserikali za Sports Development Aid (SDA) ya Lindi Mjini na Liike Finland ya Helsinki nchini Finland , ilitolewa hatua ya robo fainali ya michuano hiyo kwa penati 2-0 dhidi ya Gnistan FC baada ya sare ya mabao 3-3.
Mkurugenzi wa SDA, Mohamed Chigogolo, alisema kuwa msafara wao wa wachezaji 12 na viongozi wawili, umeondoka jijini Helsinki jana kwa ndege ya Shirika la Uturuki (Turkish Airline), ambapo watapitia jijini Istanbul, Uturuki watakounganisha ndege ya shirika hilo hilo kuja Tanzania.
Chigogolo alibainisha kuwa, wanatarajia kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 10 alfajiri kwa saa za Afrika Mashariki, ambapo watapanda gari kurejea Kilwa yaliko Makao Makuu ya FC Vito iliyokuwa moto wa kuotea mbali mashindanoni, kabla ya kukwama robo fainali.
FC Vito iliondoka nchini mwishoni mwa mwezi uliopita, ambapo iliagwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), ambaye pia Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, hafla iliyofanyika Ubalozi wa Finland nchini Tanzania .
Zaidi ya timu 1,200 za vijana chini ya miaka 11 zilishiriki michuano hiyo ya nne kwa ukubwa miongoni mwa michuano ya vijana barani Ulaya, iliyofikia tamati juzi Ijumaa, ambako Tanzania iliwakilishwa na FC Vito Kilwa iliyotinga robo baada ya kumaliza kinara wa kundi B11/J na kisha kushinda mechi ya hatua ya mtoano.

No comments:
Post a Comment