Mshambuliaji wa Yanga, Malimi Busungu (kifua wazi) akipongezwa na mchezaji mwenzake, Deus Kaseke, baada ya kuifungia timu yake bao la pili katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliomalizik jioni hii kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Katika mchezo huo Yanga ilishinda mabao 2-0, la kwanza likifungwa na Amis Tambwe katika dakika ya 44 kipindi cha kwanza na la pili likifungwa na Busungu Dakika ya 79. Aidha katika mchezo huo beki wa Yanga, Mbuyu Twite alipewa kadi nyekundu katika dakika za nyongeza baada ya kuonekana anapoteza muda wa kurusha mpira.
*********************************************
Na Ripota wa Sufianimafoto, Taifa Dar
MSHAMBULIAJI wa Yanga, Malimi Busungu, katika mchezo wa leo ameonyesha kuwa anastahili kuwa katika First Eleven ya timu yake baada ya kuonyesha uwezo wa hali ya juu alipoingia akitokea Benchi kuchukua nafasi ya Simon Msuva, ambaye leo alionekana kutokuwa vizuri kimchezo.
Busungu, baada ya kuingia alitoa pasi ya bao la kwanza lililofungwa na Amis Tambwe katika dakika ya 44, na baadaye kuifungia timu yake katika dakika ya 79 na kuiwezesha kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Simba SC katika mchezo uliomalizika jioni hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wachezaji wa Yanga wakimpongeza Busungu baada ya kutupia bao la pili.
Tambwe alifunga bao hilo baada ya kuonyesha uwezo wa pelee akigeuka baada ya kupokea pasi ya Malimi Busungu aliyepokea krosi ya Haruna Niyonzima na kumchambua kipa Peter Manyika.
Pamoja na kumaliza dakika 45 za kwanza wakiwa wanaongoza, Yanga SC bado walikuwa wakionekana kuchachawa na kuharibu pasi mara kwa mara huku Simba wakionekana kujiamini zaidi katika kipindi cha kwanza huku wakikoswa mabao mawili ya wazi. KUSOMA ZAIDI BOFYA READ MORE
Simba SC walitawala mchezo kipindi cha kwanza na kuwafanya Yanga SC kupoteana uwanjani, kiasi cha kucheza kwa kujihami muda mwingi.
Dakika ya kwanza tu, Mwinyi Kazimoto alitia krosi maridadi, lakini mshambuliaji Hamisi Kiiza ‘Diego’ akachelewa na kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ akadaka.
Beki Mkongo wa Yanga SC, Mbuyu Twite alifanya kazi nzuri dakika ya tano, baada ya kuokoa krosi nzuri ya beki wa kulia wa Simba SC, Hassan Kessy.
Dakika ya tisa, Nahodha wa Simba SC, Mussa Hassan Mgosi alishindwa kumalizia kazi nzuri ya kiungo Mwinyi Kazimoto na dakika ya 24 Kiiza alifumua shuti kali baada ya pasi ya Said Ndemla na Nahodha wa Yanga SC, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akaokoa
Mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma (kushoto) akimili mpira huku akizongwa nabeki wa Simba Hassan Isihaka.
Mashabiki wa Yanga (pichani juu) wakionyesha alama inayotumiwa na Chama cha Siasa UKAWA, huku Mashabiki wa Simba (pichani chini) nao wakionyesha alama hiyo, haikuweza kufahamika walikuwa wakimaanisha nini
Beki wa Yanga, Mbuyu Twite, aliyepewa kadi nyekundu baada ya kuchelewa kurusha mpira.
Haruna Niyonzima, akimtoka kiungo wa Simba, Said Ndemla.....
**********************************
Shambulizi la kwanza la Yanga SC lilikuja dakika ya 41, baada ya Tambwe kupiga shuti lililopanguliwa na mlinda mlango wa Simba, Peter Manyika
Kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm alimtoa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita, Simon Msuva dakika ya 34 na kumuingiza Malimi Busungu aliyekwenda kuongeza uhai katika safu ya ushambuliaji ya Yanga SC.
Kipindi cha pili Yanga SC walibadilika na kuanza kushambulia moja kwa moja, huku Simba SC nao wakiendelea kuzuia na kusaka bao la pili.
Lakini ni nyota ya vijana wa Jangwani iliyoendelea kung’ara baada ya kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 79 kupitia kwa Busungu aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa kurushwa wa Mbuyu Twite.
Baada ya bao hilo, Simba SC walipoteana na kuwaacha Yanga SC kutawala zaidi mchezo.
Kuingia kwa mshambuliaji Msenegali, Pape Abdoulaye N’daw kidogo kuliipa uhai safu ya ushambuliaji ya Simba SC na kuanza kufika langoni mwa Yanga SC, ingawa hawakufanikiwa kupata bao.
Refa Nkongo alimuonyesha kadi ya pili ya njano Mbuyu Twite dakika ya 90+2 kwa kujichelewesha kurusha mpira na Simba SC walitumia dakika hizo za majeruhi kufanya shambulizi moja la maana langoni mwa Yanga SC.
Ushindi huo, unaifanya Yanga SC ijinafasi kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ikitimiza pointi 12 baada ya mechi nne, wakati Simba SC inaanza kuporomoka.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Mwinyi Kazimoto, Kevin Yondan, Thabani Kamusoko, Simon Msuva/Malimi Busungu dk34, Salum Telela/Said Juma ‘Makapu’ dk82, Amissi Tambwe/Deus Kaseke dk87, Donald Ngoma na Haruna Niyonzima.
Simba SC;Peter Manyika, Hassan Kessy/Pape Abdoulaye N’daw dk84, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Juuko Murushid, Justice Majabvi, Awadh Juma, Said Ndemla, Hamisi Kiiza, Mwinyi Kazimoto na Mussa Hassan Mgosi/Ibrahim Hajib dk62. PICHA ZAIDI ZA MATUKIO YA MCHEZO HUU ZITAWAJIA HAPO BAADAYE
No comments:
Post a Comment