Waziri wa Kilimo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba (kushoto) akimkabidhi Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' leo jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baada ya mchezo wao dhidi ya Ndanda FC uliomalizika kwa sare ya 2-2.

Mabingwa wakishangilia baada ya kukabidhiwa Kombe lao.
Donald Ngoma (kushoto) akipongezana na mfungaji mwenzake katika mchezo wa leo, Simon Msuva.
*************************************
Na Ripota wa Mafoto Blog Dar
MABINGWA wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2016/2017 Yanga SC leo wamekabidhiwa kombe lao la ushindi huku wakilazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na Ndanda FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliomalizika jioni ya leo kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Yanga wamekabidhia kombe lao huku wakiwa na mchezo mmoja mkononi na wakiwa tayari wana jumla ya pointi 72 baada ya kucheza mechi 29,ambao mchezo wao wa mwisho utapigwa wiki ijayo huko Mjini Songea na Wana Lizombe Maji Maji.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na Selemani Kimigani wa Morogoro, aliyesaidiwa na washika vibendera Kudra Omary wa Tanga na Abdallah Rashid wa Pwani, hadi mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa mabao 2-1.
Ndanda ndiyo waliotangulia kupata bao kwa penalti dakika ya 29, mfungaji Omary Mponda aliyemchambua vizuri kipa wa Yanga, Deo Munishi ‘Dida’ baada ya beki Juma Abdul kumuangusha mshambuliaji Atupele Green kwenye eneo la hatari.
Yanga walisawazisha bao hilo dakika ya 36 kupitia kwa mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Simon Msuva kwa shuti kali akimalizia krosi ya winga Geoffrey Mwashiuya.
Mshambuliaji hatari kutoka Zimbabwe, Donald Ngoma akaifungia Yanga bao la pili dakika ya 41 kwa shuti kali pia akimalizia krosi ya beki wa kushoto, Mwinyi Hajji Mngwali.
Kipindi cha pili, timu zote zilianza na mabadiliko, Yanga wakimpumzisha Mwinyi Mngwali na kumuingiza Oscar Joshua na Ndanda wakimpumzisha Riffat Hamisi na kuingia Ahmed Msumi.
Mabadiliko hayo yaliinufaisha Ndanda iliyopata bao la kusawazisha dakika ya 79 lililofungwa na Minely aliyemalizia pasi ya Atupele Green.


No comments:
Post a Comment