Habari za Punde

*BALOZI IDDI ATEMBELEA KUKAGUA MRUNDIKANO WA MAKONTENA BANDARINI

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akifanya ziara fupi ya kukagua mrundikano wa Makontena uliopo hivi sasa katika Bandari ya Malindi Mjini Zanzibar.  Kulia ya Balozi Seif ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar, Abdulla Juma Abdulla na Meya wa Manispaa ya Zanzibar Mstahiki Khatib Abdulrahman Khatib.
 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Nd. Abdulla Juma Abdulla wa kwanza kutoka Kushoto akimueleza Balozi Seif wa Pili kutoka Kulia changamoto wanazopambana nazo watendaji wa Bandari ikiwemo mrundikano wa Makontena.  Wa kwanza kutoka Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Bandari Nd. Salmin Senga Salmin na kushoto ya Mkurugenzi wa Bandari ni Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Balozi Ali Abeid Aman Karume na Naibu Waziri wake Mh. Mohammed Ahmed Salum.
 Baadhi ya mrundikano mkubwa wa Makontena uliopo katika eneo la Bandari ya Malindi Mjini Zanzibar ukileta usumbufu kwa watendaji wa Shirika la Bandari wanaotoa huduma katika eneo hilo
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuagiza Uongozi wa Shirika la Bandari Zanzibar kuchuwa jitihada za dharura katika kukabiliana na changamoto ya msongamano wa ongezeko  kubwa la makontena ya mizigo liliopo katika Bandari ya Malindi hivi sasa.
Alisema ni vyema jitihada hizo pamoja na kufikiria hatua za kudumu za kukabiliana na tatizo hilo zikalenga pia kulitumia eneo la Bwawani kuweka makontena baada ya muwekezaji wa mradi wa Bwawani kuridhia kuruhusu kufanyika kwa kazi hiyo katika kipindi cha miezi sita.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo alipofanya ziara fupi kujionea hali halisi ya mrundikano wa makontena katika Bandari Kuu ya Malindi Mjini Zanzibar ambao unaendelea kuwaathiri wafanyabiashara mbali mbali pamoja na wawekezaji wa vitega uchumi wanaoamua kuweka miradi yao ya kiuchumi hapa Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  aliutahadharisha Uongozi wa Shirika la Bandari Zanzibar  pamoja na Bodi ya Shirika hilo kufahamu wazi kwamba wafanyabiashara wengi nchini wataendelea kulalamika huduma zinazotolewa  na Bandari hiyo kutokana na kuchelewa kwa mizigo yao.
Alisema Wafanyabiashara walioagiza bidhaa zao nje ya nchi katika kipindi hichi wamejipangia kuiuza ndani ya mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa ajili ya kujiandaa na Siku Kuu ya Iddi El – Fitri.
“ Uongozi wa Bodi sambamba na Shirika la Bandari Zanzibar ni Taasisi ambazo lazima ziende na wakati kulingana na changamoto zinazoikabili shughuli za kila siku a Bandari ”. Alisema Balozi Seif.
Balozi Seif alifahamisha kwamba msongamano uliopo kwa sasa ndani ya Bandari hiyo umekua ukiathiri mfumo mzima wa utendaji kazi ndani ya bandari hiyo sambamba na kuparaganya ratiba za meli zilizojipangia kuteremsha mizigo katika Bandari hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuonya Uongozi wa Shirika la Meli la Zanzibar pamoja na Bodi yake kuelewa kwamba kushindwa kupatikana kwa njia mbadala ya kukabiliana na mrundikano huo wa Makontena utawapa mwanya wafanyabiashara pamoja na Meli kufikia hatua ya kufatua Bandari nyengine zitakazokua na uwezo wa kuwahudumia kwa wakati unaofaa.
Akizungumzia udhibiti wa Makontena matupu yaliyokwishatolewa mizigo ndani ya Bandari hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliushauri Uongozi wa Bandari kuongeza kodi kwa meli zinazoamua kuweka Makontena yao kwa kipindi kirefu kitendo ambacho kinanyia nafasi kwa makontena yanayohitajika kuteremshwa na meli zinazofunga gati.
Alisema kiwango kinachotozwa kwa sasa kwa kila kontena moja cha Dola 40 kwa siku kinatoa fursa kwa wamiliki wa meli nyingi kuwacha makontena yao  kwa kipindi kirefu jambo ambalo huleta usumbufu kwa watendaji wa Shirika hilo.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Nd. Abdulla Juma Abdulla alisema ufinyu  wa nafasi za kuweka makontena katika eneo la Bandari umechangia kufunga gati kwa meli moja ya mizigo huku  meli nyengine zikilazimika kutia nanga zikisubiri kushusha mizigo kwa kipindi kilicho nje ya ratiba za mwenendo wa meli hizo.
Nd. Abdulla alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba baadhi ya wakati  meli za kigeni zilizobeba  mizigo ya wafanyabaishara wa Zanzibar  kwa kuharakisha ratiba zao za kazi kuamua mizigo hiyo kuiteremsha katika Bandari ya Dar es salaam.
Alifahamisha kwamba changamoto kubwa inayoikabili Bandari ya Malindi kutokana na ongezeko la meli za mizigo inayochangia harakati za uteremshaji na ushushaji wa mizigo litamalizika baada ya kufanikiwa kwa radi wa ujenzi wa Bandari ya Mpiga duri.
Naye kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya shirika la Bandari Zanzibar Nd. Salmin Senga Salmin alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  imetenga eneo maalum kwa ajili ya uhifadhi wa makontena matupu katika eneo la Saateni kwa lengo la kupunguza msongamano wa makontena katika eneo la Bandari ya Malindi.
Hata hivyo Nd. Senga alisema kulingana na mabadiliko ya harakati za kiuchumi hali ya bara bara iliyokuwa ikitumika kupitishia magari yanayochukuwa makontena hayo kutoka Bandarini hadi Saateni haikidhi hali halisi ya kupitishia mizigo hiyo.
Watendaji wa Shirika la Bandari Zanzibar wana uwezo wa kuhudumia upakuzi wa makontena elfu mbili tu kwa siku kati ya makontena elfi sita yanayohitaji kuhudumiwa kulingana na harakatiu za meli za mizigo zinazoingia na kutoka katika bandari ya Malindi.
Hivi sasa zipo meli saba za mizigo zilizotia nanga pembezoni mwa Bandari ya Malindi zikisubiri kupata huduma za kuteremsha mizigo yao katika Bandari Kuu ya Malindi.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.