Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo limepitisha muswada wa sheria ya Fedha ya mwaka 2016 ili kuwezesha utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Muswada huo umepitishwa na Bunge pamoja na marekebisho yake ambayo yametolewa na kamati ya kudumu ya bunge ya bajeti na wabunge.
Marekebisho yaliyofanyika katika muswada huo ni pamoja na kutoongeza ushuru wa kuingiza sukari ya viwandani kutoka asilimia 10 kwenda 15 ambapo kamati ya kudumu ya bunge ya bajeti ilishauri Serikali isiendelee na pendekezo hilo kutokana na hatua hiyo kuwa na athari kwa viwanda vinavyotumia sukari viwandani kama malighafi ya kuzalisha bidhaa nyingine kama juisi na soda.
“Serikali imekubali pendekezo lililotolewa na kamati ya kudumu ya Bunge ya bajeti ya kutoongeza ushuru wa kuingiza sukari ya viwandani kutoka asilimia 10 kwenda asimilia 15, hivyo kuendelea kutoza asilimia 10 iliyokuwepo kwa mwaka huu wa fedha,” alifafanua Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango.
Marekebisho mengine yaliyofanyika ni pamoja na kuondoa adhabu ya kifungo cha miezi Sita kwa wale ambao hawatodai risiti baada ya kununua bidhaa au huduma na kubaki na adhabu ya kulipa faini kulingana na thamani ya bidhaa.
Aidha Mhe. Mpango amesema kuwa muswada huo umezingatia kwa kiwango kikubwa mapendekezo ya wadau mbalimbali wakiwemo wabunge, wamiliki wa viwanda, wafanyabiashara na taasisi za Serikali.
No comments:
Post a Comment