MJUMBE wa Bodi ya Kituo cha Ufundi cha Kilimo na Maendeleo Vijijini (Technical Centre for Agricultural and Rural Cooperation, CTA) chenye makao makuu mjini Wageningen, Uholanzi, Prof. Faustin Kamuzora, akikabidhi kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete uteuzi wa kuwa Balozi wa Heshima (Goodwill Ambassador) wa Maendeleo ya Kilimo katika Mabara ya Afrika, Karibiani na Pasafiki, uliofanywa na Kituo hicho cha CTA, Pfrof. Kamuzora aliwasilisha uteuzi huo, alipokwenda Ofisini kwa Dk. Kikwete, katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jinini Dar es Salaam, juzi. Picha na Bashir Nkoromo.
*************************************************
NA BASHIR NKOROMO
KITUO cha Ufundi cha Kilimo na Maendeleo Vijijini (Technical Centre for Agricultural and Rural Cooperation, CTA) chenye makao makuu mjini Wageningen, Uholanzi kimemteua Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete kuwa Balozi wa Heshima (Goodwill Ambassador) wa Maendeleo ya Kilimo katika Mabara ya Afrika, Karibiani na Pasafiki.
Katika barua iliyokabidhiwa na mjumbe wa Bodi ya CTA, Prof. Faustin Kamuzora, CTA wameainisha kuwa Dk. Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, Taifa, ameteuliwa kwa kutambua mchango wa juhudi zake katika kukiendeleza kilimo nchini Tanzania na barani Afrika.
Katika wadhifa wake huo mpya, CTA imemuomba Dk. Kikwete aweze kuiwakilisha katika makongamano ya kimataifa ambapo atazungumzia umhimu wa kukiendeleza kilimo kwa ajili ya kutoa fursa ya ajira zenye staha kwa vijana na wanawake katika nchi za barani Afrika, Karibiani na Pasifiki. Pia ataisaidia CTA katika kuandaa makala na kufanya mahojiano na waandishi wa habari katika nchi mbalimbali.
Dk. Kikwete amekubali uteuzi huo na kuahidi kushirikiana na CTA katika kutekeleza mambo ambayo ameombwa kuisaidia na taasisi hiyo ambayo ni ushirikiano wa Umoja wa Ulaya na Kundi la nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki wenye makao makuu mjini Brussels, Ubelijiji.
Prof. Kamuzora ambaye pia ni Katibu Mkuu, Mawasiliano ni mjumbe wa Bodi ya CTA akiwakilisha nchi za ukanda wa Afrika Mashariki kwa miaka mitano tangu 2013 hadi 2018.
No comments:
Post a Comment