Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Mhe.Dkt.Abdallah Possi akichukua dondoo za Mkutano wa 9 wa nchi ambazo zimeridhia Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu uliofanyika katika Ukumbi wa Umoja wa Mataifa Marekani.
Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano wa 9 wa nchi ambazo zimeridhia Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu wakifuatilia mada wakati wa mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Umoja wa Mataifa New York Marekani.
*******************************************
Na Mwandishi Wetu
Siku ya tarehe 15 Juni, 2016, Mhe. Dkt. Abdallah Possi (MB), Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu alishiriki katika Mjadala wa kutokomeza umasikini na kuleta usawa kwa watu wenye ulemavu. Majadiliano hayo yalikuwa ni moja ya mikutano muhimu iliyolifanyika katika Mkutano wa 9 wa nchi ambazo zimeridhia Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu uliofanyika New York, Marekani.
Mwenyekiti wa majadiliano hayo alikuwa ni Bi. Ellen Maduhu, Afisa katika ofisi ya uwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa ambaye pia ni Makamu wa Raisi wa Kamati ya Mkutano wa Nchi ambazo zimeridhia Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (Vice President of the Conference of State Parties to the Convention on the Rights of Persons of Disabilities)
Mhe. Dkt. Possi alikuwa ni mmoja wa watoa mada aliyeliwakilisha bara la Afrika. Katika majadiliano hayo kulikuwa na watoa mada wengine watano kutoka mataifa mengine wakiwemo Ms. Asa Regner, Waziri wa watoto, wazee na usawa wa kijinsia kutoka Sweden; Bw. Joelson Dias, mjumbe wa Kamati maalumu inayoshughulikia haki za watu wenye ulemavu, Brazil; Bi. Silvia Quan kutoka Taasisi ya Haki za Binadamu wakiwemo watu wenye ulemavu, Brazil; Ms. Mercedes Juan, kutoka Kamisheni ya Taifa kwa ajili ya maendeleo na ujumuishwaji wa wenye ulemavu, Mexico; na Bi. Emi Aizawa kutoka Taasisi ya Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA)
Katika Majadiliano hayo, watoa mada walilenga hoja zao katika kujibu maswali ya mambo makuu matatu.
Jambo la kwanza lilikuwa kuelewa hatua zilizochukuliwa na nchi husika na wadau wengine kupunguza umaskini na kukosekana kwa usawa kwa watu wenye ulemavu.
Jambo la pili lilikuwa kujua hatua zilizochukuliwa na nchi husika na wadau wengine katika kuhakikisha masuala muhimu ya watu wenye ulemavu yanaingizwa katika sera zao za kitaifa za maendeleo na mipango ya kuondoa umasikini na kuhakikisha usawa katika jamii.
Suala la tatu lilikuwa kuelewa hatua zilizochukuliwa na wadau mbalimbali katika kuhakikisha kwamba mipango ya maendeleo endelevu ya ajenda 2030 yanajumuisha masuala muhimu ya kuwakomboa watu wenye ulemavu kwa kuwaletea maendeleo na usawa.
Katika mada yake, Mhe. Dkt. Possi alieleza kuwa katika kuhakikisha Tanzania inatoa haki na usawa kwa watu wenye ulumavu, Serikali imetengeneza sheria, sera na miongozo mizuri ya kusimamia usawa miongoni mwa watu wenye ulemavu.
Alibainisha kuwa sera na Sheria nzuri zilizopo zinakabiliwa na changamoto mbali mbali katika utekelezaji wake ikiwa ni pamoja na changamoto za kiuchumi. Hata hivyo, Serikali imejipanga kukabiliana na changamoto hizo.
Vile vile Mhe. Possi alieza kuwa uchumi duni katika nchi nyingi zinazoendelea umekuwa chanzo kikubwa cha kudhoofisha jitihada za kuleta maisha bora kwa watu wenye ulemavu.
"Tanzania, kama mataifa mengine yanayoendelea, inakabiliwa na changamoto za kiuchumi ambazo zinaathiri maisha ya watu wenye ulemavu, kama vile upatikanaji wa maji safi, chakula, afya na elimu. Pia kuna tatizo la jumla la ukosefu wa ajira, ambayo pia huathiri watu wenye ulemavu", alieleza Mhe. Possi.
Dkt. Possi pia aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa mitazamo hasi ya kijamii, na ukosefu wa vifaa muhumu vya kuwasaidia watu wenye ulemavu (assistive devices) vinachangia kwa kiasi kikubwa kwa watu wenye ulemavu kutoshirikishwa katika masuala ya jamii ikiwa ni pamoja na shughuli za kiuchumi.
Tatizo la upatikanaji wa vifaa kwa watu wenye ulemavu limekwamisha maendeleo na ustawi bora wa watu wenye ulemavu hapa nchini, hususani kwa wale wenye kipato cha chini.
"Kikwazo kikubwa kwa Tanzania ni ukosefu wa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu, hali hii inazuia Watu wenye Ulemavu kuendelea, kwa sababu bila ya vifaa saidizi, Watu Wenye Ulemavu hawawezi kupata huduma muhimu za kijamii kama elimu na mafunzo kwa ajili ya maisha ya kujitegemea na mchango wa mchakato wa maendeleo wa taifa lao. Hii inajenga kikwazo kingine cha ajira na bila kuwa na ajira yenye kipato, watu wenye ulemavu wataendelea kubaki maskini," alisisitiza Dkt. Possi.
Mwisho, Dkt. Possi alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuzisaidia nchi kama Tanzania katika kupata vifaa saidizi vya watu wenye ulemavu, ikibidi kupata teknolojia ya kuvitengeneza vifaa hivyo ndani ya nchi ili vipatikane kwa urahisi.
No comments:
Post a Comment