Na Zainab Nyamka, Dar
BAADA ya kutokutumia jezi zenye mdhamini
wao bia ya Kilimanjaro, Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) limetolea ufafanuzi
kuhusiana na suala hilo kwani kutokana na kanuni za michuano ya Shirikisho la
Soka Afrika (CAF) kuwa timu yoyote inapoingia kwenye hatua ya makundi (nane
bora) haki za udhamini za timu zote zinahamia kwa shirikisho hilo kwa hiyo
wadhamini wote wanatakiwa kuingia makubaliano na CAF na si klabu tena.
Akizungumza na waandishi wa habari Afisa habari wa TFF, Alfred Lucas
amefafanua hayo mapema leo na kusema kuwa, Yanga hawakuhudhuria vikao vya
awali vya timu zilizoingia kwenye hatua ya makundi kama walivyotakiwa na ndiyo maana
hawakulifahamu hilo ila kwa sasa kama mdhamini atataka aendelee kuweka nembo
atatakiwa kukaa chini na CAF na kukubaliana.
“Timu yeyote ikifika hatua ya
makundi haki za udhamini zote zinahamia kwa CAF, na zaidi Yanga wanaweza
kuendelea kutumia jezi zao mpya kama Bia ya Kilimanjaro hawatataka kuweka nembo
yao tena.”
Kwa upande wa klabu ya Yanga, Mkuu wa
kitengo cha Haabari na Mawasiliano Jerry Muro amesema kuwa mkataba wao na Bia
ya Kilimanjaro unaelekea ukingoni na kusema kuwa ni uamuzi wao kutaka kuendelea nao au
kuangalia uwezekano wa kupata kampuni nyingine itakayokuwa na maslahi zaidi na
itakayoinufaisha klabu yao.
Aidha alisema kuwa wakati wanaenda nchini Algeria hawakuwa
wakifahamu kuwa kama kuna mabadiliko ya jezi kwani hawakuhudhuria kikao cha
awali cha timu zilizoingia kwenye hatua ya makundi.
”Kutokana na kutojua
mabadiliko ya kanuni za CAF kuwa haki za udhamini zinahamia kwao na Klabu yeyote haitaruhusiwa kutumia nembo ya mdhamini mpaka watakapokubaliana nao,
hata hivyo udhamini wetu na Bia ya Kilimanjaro, unamalizika hivi karibuni hivyo tutaangalia kampuni itakayohitaji kushiriki nasi na maslahi zaidi,
Mpaka sasa yameshajitokeza makampuni
mengi, ila bado wapo kwenye mazungumzo na masuala yote yakikamilika basi tutawataarifu mashabiki na wanachama wa Yanga kuhusiana na
ujio mpya wa mdhamini'' alisema Muro.
Yanga kwa sasa wataendelea kutumia jezi hizo kwenye michuano ya
Kombe la Shirikisho na kuna uwezekano wa kuzitumia mpaka kwenye ligi kuu
msimu ujao. Kampuni hiyo ya Macron iliyopo nchini Italia inayotengeneza jezi hizo, imeingia mkataba na Yanga wa kuwavalisha kuanzia sasa huku ikiwa tayari inawavalisha
mabingwa wa kihistoria Afrika Zamaleck ya nchini Misri.
Muro amesema, wanataka kuwa tofauti na
wengine kuanzia mavazi hado utofauti wa kuendesha timu yao kwani hadi sasa wao
ndiyo wawakilishi pekee wa Afrika Mashariki na Kati na wanataka kuhakikisha
wanafika mbali zaidi na kuweka historia nchini. Ukiachilia mbali hilo amewataka
mashabiki wa Yanga kuendelea kuisapoti timu yao kuelekea mchezo wao wa pili dhidi
ya Tp Mazembe utakaopigwa Juni 28 Jijini Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment