Na Zainab Nyamka, Dar
KIKOSI cha Yanga kinarejea wakati wowote kuanzia kesho kutoka nchini Algeria baada ya kumaliza mchezo wao wa kwanza wa kombe la Shirikisho dhidi ya Mo Bejaia uliomalizika kwa mabingwa hao wa Ligi kuu Bara kupoteza kwa goli 1-0.
Yanga wameamua kurudi nchini badala ya kurejea nchini Uturuki kuendelea na Kambi kama ilivyokuwa imepangwa kutokana na kukabiliwa na mchezo mwingine dhidi ya TP Mazembe unaotarajiwa kuchezwa Juni 28 kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es salaam, ila katika mechi hiyo watamkosa nyota wa kimataifa wa Burundi Amis Tambwe ambaye ampeta kadi mbili za njano.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro amesema kuwa wamekubali kuwa wamepoteza mchezo huo lakini hawakupendezwa na maamuzi ya mwamuzi wa kati zaidi wanategemea kufanya vizuri katika mchezo wao unapofuata dhidi ya Mazembe ambao na wao watakuwa na faida ya kuwa nyumbani. “ Tumekubali tumefungwa na zaidi goli halikuwa na matatizo yoyote yale ila tunashukuru kuwa tunajipanga kwa ajili ya mchezo wa pili ambao utakuwa nyumbani dhidi ya Mazembe ni faida kwetu kwani hatutaweza kuruhusu kupoteza katika uwanja wetu wa nyumbani,”.
Baada ya kupoteza mchezo huo, kikosi kitarejea nchini kwa ajili ya kujiandaa, na wataweka kambi hapa hapa Dar es salaam na kukosekana kwa mchezaji Amisi Tambwe haitakuwa pengo kwao zaidi nafasi yake itachukuliwa na Mshambuliaji wa Kimataifa wa Zambia aliyesajiliwa mapema wiki hii kutoka Fc Platinum ya Zimbabwe, Obrey Chirwa kama usajili wake utapitishwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Akizungumzia kuhusiana na usajili wa Hassan Kessy ambaye ameshindwa kucheza katika mchezo wa jana dhidi ya Mo Bejaia kwa madai kuwa Klabu ya Yanga walizembea kwenda kuchukua barua ya kumruhusu mchezaji huyo kutoka kwa Mahasimu wao Simba, Muro alisema kuwa wanachokijua wao kuwa Simba hawakutoa barua hiyo na zaidi walifanya hivyo kuwakomoa wao ila watambue kuwa kila lenye mwanzo lina mwisho na ipo siku watakuja kujutia kitendo walichokifanya.
“Tumepata salamu zao kuwa sisi hatukwenda kuchukua barua ya Simba ila ukweli uko wazi kuwa wao ndiyo wametufanyia figisufigisu za makusudi kushindwa kutupatia barua hiyo ya kuidhinisha kucheza ila watambue kuwa ipo siku watakuja kujutia kitendo hicho ila siku zote wafahamu kuwa wao wanajua kukimbia ila njia hawaijui, na sisi tunajua kukimbia na njia tunaijua.'' alisema Muro
No comments:
Post a Comment