Na Zainab Nyamka, Dar
BAADA ya msimu wa ligi Kuu Bara kumalizika hadi sasa bado baadhi
ya timu zipo katika mapumziko na nyingi zikiwa bado katika mchakato wa usajili.
Lakini hili ni tofauti kwa upande wa timu ya Ruvu Shooting
ambao wamerejea tena Ligi Kuu msimu ujao baada ya kupanda huku wakiongoza
katika Kundi B.
Ruvu Shooting wao licha ya kuwa ni mwezi mtukufu, wao tayari
wameingia Kambini na tayari wameanza kujifua kwa kasi kuelekea msimu ujao wa
Ligi Kuu Tanzania Bara .
Akizungumza na mtandao huu, Mafoto Blog, Afisa habari wa
timu hiyo, Masau Bwire amesema kuwa timu yao
tayari imeingia Kambini na imeanza mazoezi licha ya kuendelea kwa mwezi mtukufu
wa ramadhani, na kusema kuwa msimu ujao ni muhimu sana kwao kwani wanataka
kudhihirisha kuwa walifanyiwa hujuma za kushushwa daraja msimu wa 2014/15.
Masau alisema kuwa timu yao bado inakikosi bora ndio maana
wamefanikiwa kurudi Ligi kuu wakiwa na alama ambazo hazikuweza kufikiwa na timu
yeyote ndani ya kundi lao.
"Tunataka kuwashangaza mashabiki wa soka nchini na
tumejipanga kuchukua Ubingwa msimu uajao kama walivyofanya, Leicester City, Tunajua
kuwa mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhani ni ibada muhimu lakini pia haiwazuii
wachezaji kufanya mazoezi au kazi nyingine ambazo ni muhimu kwao", amesema
Masau.
Aidha amesema kuwa kuelekea msimu ujao wa ligi kuu mwalimu
wa timu hiyo, Tom Olaba anataka kufanya mabadiliko ya kikosi chake kwa
kukiongezea nguvu katika baadhi ya maeneo kwani mapendekezo yake ni kuongeza wachezaji saba wa nafasi
mbalimbali na alishapeleka suala hilo kwa uongozi.
Masau amesema kuwa timu hiyo itafanya usajili kutokana na
mapendekezo ya mwalimu huyo ambayo yataungwa mkono kwa asilimia mia moja.
No comments:
Post a Comment