Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Manispaa ya Ilala kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Korea (KOICA) inatarajia kutumia kiasi cha shilingi bilioni 18 kukamilisha Ujenzi wa Hospitali ya kisasa ya kutolea huduma za matibabu kwa mama na mtoto katika Kata ya Chanika,wilayani Ilala.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Afisa Habari wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, David Langa wakati akitoa ufafanuzi kuhusu maboresho yanayofanywa katika Sekta ya Afya ndani ya Manispaa hiyo.
Amesema hospitali hiyo itakamilika mwishoni mwa mwaka huu na kuongeza kuwa itakuwa na vitanda 266 pamoja na mashine zote za upasuaji na matatibu ya magonjwa yote ya wanawake na watoto.
“Ujenzi wa Hospitali hii kubwa ya wanawake na watoto unaendelea, tutatumia shilingi bilioni 18 kukamilisha kazi ya ujenzi na kuweka vifaa vya kisasa”,amesema Langa.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana, Dkt. Meshach Simwela amesema kuwa hospitali hiyo itakapokamilika itakuwa na vifaa vya kisasa pamoja na madaktari bingwa kutoka hospitali ya Taifa Muhimbili, Amana, Mnazi Mmoja pamoja na hospitali nyingine za Serikali.
“Mpaka sasa jumla ya waganga watano na wauguzi sita wameshapelekwa Korea kujifunza namna ya kutoa huduma na jinsi ya kutumia vifaa vipya vitakavyoletwa mara baada ya Hospitali hii kukamilika”, alisema Simwela.
Ameongeza kuwa ujenzi huo unategemewa kukamilika mwaka huu na unategemewa kufunguliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli au Makamu wa Rais Mhe.Mama Samia Suluhu kwa kuwa ni Hospitali ya kwanza nchini Tanzania kuwa na hadhi kubwa kama hiyo.
No comments:
Post a Comment