Habari za Punde

*WATANZANIA KUMILIKI HISA KATIKA KAMPUNI ZA MAWASILIANO ZA HAPA NCHINI

 Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Serikali kufanya marekebisho ya Sheria ya Posta na Mawasiliano ya Kieletroniki ili kuwezesha watanzania kumiliki hisa zitakazouzwa na Kampuni za Mawasiliano kupitia soko la hisa.
Hayo yamesemwa leo Bungeni  Mjini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango alipokuwa akiwasilisha Bungeni  muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2016. 
“Mhe. Naibu Spika, sehemu ya nne inapendekeza marekebisho katika sheria ya Posta na   Mawasiliano ya Kielektroniki, sura 306 kama ifuatavyo, kufuta kifungu cha 6(2d) na kukiandika upya ili kuweka sharti kwa kampuni za mawasiliano kuwasilisha Katiba ya Kampuni itakayothibitisha muundo wa umiliki wa hisa kama mojawapo ya taarifa zinazopaswa kuwasilishwa wakati wakuomba leseni,” alifafanua Mhe. Mpango.
Aidha Mhe. Mpango aliendelea kwa kusema kwamba, watoa huduma za Mawasiliano ya Kielektroniki watawekewa sharti la kuuza hisa zao kwa Umma na kusajili hisa zao katika soko la hisa Nchini Tanzania ili kutoa fursa kwa watanzaniai kununua hisa na kumiliki asilimia 25 ya Kampuni hizo.
Kutokana na marekebisho ya sheria hiyo, kampuni za huduma za Mawasiliano ya kielektroniki ambazo tayari zimesajiliwa hapa Nchini zitawajibika kujioredhesha katika soko la hisa na kuuza hisa zao ndani ya kipindi cha miezi sita kuanzia Julai 01, 2016.
Vile vile kampuni ambazo zitasajiliwa baada ya Julai 01, 2016 zitawajibika kuuza hisa zao na kujioredheshsha katika soko la hisa ndani ya kipindi cha Miaka miwili kuanzia Julai 01, 2016.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti  Mhe. Hawa Ghasia amesema kwamba kamati imekubaliana na marekebisho hayo aidha kamati inaishauri Serikali  kuweka tafsiri ya watanzania ili kuwezesha hisa hizo kuuzwa kwa watanzania  pekee na pia kuangalia suala la miezi sita kwa makampuni yaliyosajiliwa lisilete utata kwenye utekelezaji wake.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.