Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
WAFANYABIASHARA wa Tanzania wametakiwa kutumia fursa za biashara zinazopatikana katika soko la nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuuza bidhaa zao ndani ya Jumuiya hiyo.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
“Wafanyabiashara wanatakiwa kuchangamkia fursa ya biashara katika soko la pamoja kwa kuwa ni haki yao na ni utekelezaji wa malengo ya Mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kifungu cha tano ambapo ilianzishwa itifaki ya umoja wa forodha ” ,alisema Bi. Mindi
Wafanyabiashara hao pamoja na wasafirishaji wanaotaka kufanya biashara katika soko la Jumuiya hiyo watatakiwa kuonesha cheti cha uasilia wa bidhaa wakati wakiingia nchi wananchama wa Jumuiya hasa kwa wafanyabiashara wadogo wenye bidhaa zisizozidi dola za kimarekani 2000, ambapo hawalazimiki kuwa na wakala wa forodha.
Wanatakiwa kufuata utaratibu kwa kufika katika kituo chochote cha forodha kilichopo mpakani wakiwa na bidhaa zao ili wapewe cheti cha uasilia wa bidhaa.
Naye, Mkurugenzi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji, katika Wizara hiyo, Bw. Geofrey Mwambe, amesema ni vyema wafanyabiashara wakatoa taarifa endapo watakumbana na vikwazo visivyo vya kiforodha kupitia mfumo wa ujumbe mfupi kwa kuandika neno ‘NTB’ kwenda namba 15539.
Bw. Mwambe amesema pia ,madereva wanaosafirisha mizigo kwenda nchi wanachama watakapokutana na vikwazo visivyo vya kiforodha barabarani watoe taarifa kwa Jeshi la Polisi kupitia namba 0713631780.
Kwa mujibu wa Mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kifungu namba 5 ambapo Jukuiya ilianzisha Itifaki ya Umoja wa Forodha (East African Community Customs Union) wafanyabiashara wa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo wana fursa za kufanya biashara kwa kuuza bidhaa zao ndani ya nchiwanachama wa Jumuiya hiyo ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi bila kutozwa ushuru wa forodha ilimradi bidhaa zao zimezingatia vigezo na kufuata utaratibu ulioainishwa katika itifaki hiyo.
Japokuwa Sudani ya Kusini imeridhia kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki bado fursa za kufanya biashara nchini humo hazijakamilika.
No comments:
Post a Comment