Uongozi wa Klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam, umetoa tamko kuhusu kuachwa kwa kiungo wake Salum Telela, baada ya ukimnya mwingi na maneno ya chini chini kuhusu kiungo huyo, anayeelezewa kutaka kutua kwa mahasimu wa Yanga Simba SC.
Akizungumza na mtandao huu kwa njia ya simu Msemaji wa Yanga, Jerry Muro, alisema kuwa ni kweli mkataba wa kiungo huyo umemalizika na mwezi huu na kuongeza kuwa kwa sasa mchezaji huyo yupo huru kuzungumza na timu yeyote itakayomhitaji.
Aidha kumekuwepo na maneno mengi ya chini chini kuhusu kuachwa kwa kiungo huyo wakati angali na kiwango bora kwamba kuna figisu figisu zinazoendelea baina yake na mmoja kati ya viongozi wa klabu hiyo ambaye amekuwa akimshawishi Kocha Mkuu kutomchezesha na kutomuongezea mkataba.
Kikizungumza na Mtandao huu, Chanzo cha habari hii kilisema kuwa mara kadhaa Telela alikuwa akipishana kiswahili na Kocha wake lakini kutokana na upole wake na kutokuwa mtu wa maneno wala kujibizana Kocha huyo alikuwa kijikuta akijistukia na baadaye kumfuata Telela na kumuomba msamaha baada ya kukwaruzana.
Pamoja na kuwa kiungo huyo ni kiraka mwenye uwezo wa kucheza nafasi tofauti uwanjani kama beki wa kulia, kati na nafasi zote za kiungo, lakini bado uongozi umemtosa na kutomuongezea mkataba jambo ambalo limezua gumzo miongoni mwa mashabiki wa Klabu hiyo.
Kutokana na kiungo huyo kuwa mpole na nidhamu ya hali ya juu na bidii katika mazoezi, hata wachezaji wenzake wamesikitishwa na uamuzi wa Kocha wao kutomuongezea mkataba.
Na hata baadhi ya viongozi wa Yanga bado unaonekana kupingana na maamuzi ya Pluijm kumtema Telela ambaye amedumu Yanga tangu mwaka 2011 aliposajiliwa mara ya kwanza kutoka Moro United.
No comments:
Post a Comment