Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua Mkutano wa Wadau wa Benki za Wananchi kwenye Ukumbi wa Hazina mjini Dodoma leo Juni 15, 2016
Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa Wadau wa Benki za Wananchi
wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua mkutano
wao kwenye ukumbi wa Hazina mjini Dodoma Juni 15, 2016.
Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa Wadau wa Benki za Wananchi wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua mkutano wao kwenye ukumbi wa Hazina mjini Dodoma Juni 15, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na washiriki
wa Mkatano wa Wadau wa Benki za Wananchi kwenye ukumbi wa Hazina mjini
Dodoma juni 15, 2016. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
***************************************
***************************************
Na Benny
Mwaipaja-WFP
WAZIRI MKUU, Mhe.
Kassim Majaliwa, amezishauri taasisi za fedha nchini zipunguze viwango vya riba
zinazotoza kwenye mikopo ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi hususan waishio
vijijini kujikwamua kiuchumi
Majaliwa ametoa
kauli hiyo leo Juni 15, 2016, wakati
akifungua mkutano wa wadau wa Jumuiya ya Benki za Wananchi (COBAT),
ulioshirikisha viongozi wa mikoa 28 nchini, uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano
wa Hazina Mjini Dodoma.
Waziri Mkuu Mhe.
Majaliwa amesema kuwa riba kubwa inayotozwa na taasisi hizo za fedha ni kubwa
na kuwafanya wananchi wengi washindwe kunufaika na fursa za mikopo inayotolewa,
hali inayowafanya waendelee kuwa
masikini.
"Kama Benki
zitatoa mikopo yenye riba nafuu, kila mwananchi atamudu kupata mtaji na kufanya
biashara yake akijua kuwa riba si kubwa na tayari Serikali imeanza kufanya
mazungumzo na taasisi za fedha kuhusu jambo hili ili ziweze kufanya mapitio ya
riba zake"Aliongeza Mhe. Kassim Majaliwa
Ameipa mikoa ambayo
haijaanzisha benki za wananchi-COBAT, muda wa miezi mitatu kuanzisha mchakato
huo ili kufikisha huduma rasmi za kifedha kupitia benki hizo ili kuchochea na
kuamsha uzalishaji mali wenye tija katika jamii.
Amesema lengo
muhimu la kuwainua wananchi kimaisha litatimia kwa kuhamasisha wananchi mijini
na vijijini, wenye kipato cha chini kabisa katika kujenga utamaduni wa
kujiwekea akiba na kuwekeza katika hisa ili kukuza mitaji itakayosaidia
shughuli za maendeleo kwenye maeneo yao yote.
Ameahidi kuwa
Serikali itaangalia uwezekano wa kuiwezesha mikoa itakayoonesha ari zaidi ya
kuanzisha benki zao za wananchi kwa kuzishirikisha Halmashauri za wilaya,
Manispaa, Miji na Majiji.
"Inawezekana
kabisa kuanzisha benki hizo kwa kukusanya hisa kutoka kwa wananchi na
Halmashauri zikachangia ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kufikiwa na huduma
za kibenki katika maeneo yao"Alisisitiza Waziri Mkuu.
Amesema ni matumani
ya serikali ya awamu ya tano kwamba uanzishwaji wa benki hizo una umuhimu
mkubwa kwa kuwa zitakuwa kiunganishi mahsusi ambacho kikiwa imara kitaleta
mabadiliko chanya katika kuwawezesha wananchi kujikwamua na kujiletea maendeleo
ya haraka.
Waziri wa Fedha na
Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango, ameeleza kuwa hadi kufikia mwaka 2016, mikoa
8 tu ya Tanzania bara ndiyo imeanzisha benki za wananchi-COBAT kati ya mikoa 26
iliyopo.
Amezitaja benki
hizo zilizoko chini ya Jumuiya ya Benki za Wananchi Tanzania-COBAT kuwa ni
Mucoba (Mufundi), Mbinga (Mbinga), Mwanga (Mwanga), Uchumi (Moshi), Tandahimba (Mtwara),
Meru (Arusha), Njombe (Njombe) na Efatha (Dar es salaam)
Dkt. Mpango amesema
kuwa Benki hizo zinawateja wanaokadiriwa kufikia 600,000 zikiwa na jumla ya
mali iliyofikia shilingi Bilioni 86.3 na amana za wateja shilingi Bilioni 69.2
na kutoa mikopo kwa wateja wake inayofikia shilingi Bilioni 56.2
"Mpango wa
kuhakikisha huduma za fedha zinawafikia wananchi wengi zaidi ni sehemu ya
utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya taifa inayolenga kuipeleka Tanzania katika
nchi ya kipato cha kati na yenye uchumi imara ifikapo mwaka 2015"
Amesisitiza Dkt. Mpango
Amesema hadi
kufikia Desemba mwaka 2015, Taasisi za benki za wananchi za mikoa, vyama vya
ushirika vya akiba na mikopo, zimeongezeka hadi kufikia 4,093, zikiwa na
wanachama 733,876 na kuwekeza kiasi cha shilingi Bilioni 377.6
"Aidha, Asasi
za Fedha za Kijamii (Vicoba, Vsla, Rosca), zinakadiriwa kufikia 100,000 na zina
wanachama milioni 2.2 na mtaji wa shilingi Trilioni 1.2" aliongeza Dkt
Mpango
Amesema kuwa
utafiti uliofanyika hivi karibuni na shirika la Finscope umebaini kuwa asilimia
57.4 ya watanzania wanapata huduma rasmi za kifedha, ambapo kati ya hao,
asilimia 13.9 wanapata huduma za kibenki huku asilimia 43.5 wanapata huduma za
kifedha zisizo za kibenki.
Waziri wa Fedha na
Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango, amezitaja changamoto zinazoikabili sekta ya
Fedha nchini kuwa ni upungufu wa mitaji, ukusanyaji mdogo wa amana, kiwango cha
riba kuwa juu, ushindani kutoka benki za biashara na taasisi zingine za Fedha,
kukosekana kwa wataalamu wa kuziendesha na kukosekana kwa sheria na kanuni
mahsusi kwa benki za wananchi na Ushirika.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Benki za Wananchi Tanzania-COBAT, Elizabeth Makwabe,
amesema kuwa katika kipindi cha miaka 20 sasa, benki za wananchi zimeendelea
kupanua huduma zake ambapo hadi sasa, mali, amana na mikopo vimeongezeka kutoka
shilingi Bilioni 71.2 mwaka 2014 hadi kufikia shilingi Bilioni 86.3 mwaka 2015
Ameiomba serikali
kuwekeza fedha za kutosha kwenye benki za wananchi katika mfumo wa fedha za
kuzungusha (Revolving Fund) ili kusisimua uchumi katika maeneo ya vijijini
pamoja na kuzitaka Halmashauri za wilaya kuwekeza mitaji kwenye benki hizo
katika maeneo yao.
Akitoa neno la
Shukrani kwaniaba ya wakuu wa mikoa waliohudhuria mkutano huo, mkuu wa mkoa wa
Manyara, Dkt. Joel Bendera, ameahidi kuwa mikoa yote 18 ambayo haijaanzisha
benki za wananchi itahamasisha na kuanzisha benki hizo kwa faida ya wananchi
wao.
No comments:
Post a Comment