Habari za Punde

*WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO YATOA ELIMU YA UBIA KATI YA SERIKALI NA SEKTA BINAFSI KWA WABUNGE

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Uratibu Bunge Vijana Kazi Ajira na Walemavu Mhe. Jenista Mhagama(wa kwanza kushoto) akifuatilia Semina iliyoandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango ikilenga kuwajengea uwezo wabunge kuhusu umuhimu wa kushirikiana kati ya Sekta Binafsi na ile ya Umma (PPP) Katika miradi ya maendeleo. Kulia ni Spika wa Bunge Mhe. Tulia Ackson ambaye alikuwa mgeni rasmi katika semina hiyo.
 Mbunge wa Ileje Mhe. Janet Mbene akitoa maoni yake  wakati wa semina ya kuwajengea uwezo wabunge kuhusu  umuhimu wa kushirikisha Sekta Binafsi katika miradi ya maendeleo.
 Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Sophia Simba akitoa maelezo  jinsi miradi itakayotekelezwa kwa ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi inavyoweza kuchangia kukuza maendeleo.
 Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson (katikati) ambaye alikuwa mgeni rasmi  wa semina ya kuwajengea uwezo Wabunge kuhusu umuhimu wa Ubia kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma (PPP) akifurahia jambo mapema leo Bungeni Mjini Dodoma. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Servacius Likwelile na kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bajeti Mhe. Josephat Kandege.
 Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Mhe. Josephat Kandege akiwakaribisha wajumbe kutoa maoni katika Semina iliyoandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa lengo la kuwajengea uwezo Wabunge kuhusu umuhimu wa ubia kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma. Kulia ni Spika wa Bunge Mhe. Dkt. Tulia Ackson ambaye alikuwa Mgeni Rasmi  kwenye semina hiyo. Picha na Frank Mvungi-Dodoma 
********************************
Na: Lilian Lundo – Dodoma – Maelezo
Wizara ya Fedha na Mipango leo Mjini Dodoma imetoa semina Kuhusu  ubia kati ya Sekta Umma na Sekta  Binafsi kwa wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Semina hiyo iliyofunguliwa na Naibu Spika Mhe. Tulia Ackson  ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye semina hiyo ambapo  mada  kuhusu utaratibu  huo iliwasilishwa na Kamishna anasimaia Idara inayoratibu  ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kutoka Wizara hiyo Dkt. Frank Mhilu.
“Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ni mkataba wa muda mrefu wa kuanzia miaka 5 hadi 30 na kuendelea kati ya kampuni ya mwekezaji binafsi na Taasisi ya Serikali ambapo mwekezaji binafsi anajenga miundombinu  au anapewa miundombinu ili aiboreshe kwa lengo la kutoa huduma ya umma kwa gharama nafuu  na baada ya mkataba kwisha miundombinu husika hurejeshwa kwa Serikali,” alifafanua Dkt. Mhilu.
Aidha Dkt. Mhilu aliendelea  kusema kuwa, ili kufanikiwa katika ubia lazima kuwe na maandalizi muhimu ambayo ni kuibua fursa za uwekezaji kwa mujibu wa mpango wa Taifa wa maendeleo, kufanya uchambuzi yakinifu ili kujiridhisha kuwa mradi una manufaa kwa uwekezaji kwa utaratibu wa ubia.
Vile vile kuandaa ardhi na miundombinu wezeshi, kutangaza miradi kwa uwazi, kujiridhisha ubora wa zabuni ya mwekezaji na namna ambavyo fedha zitapatikana na uwezo wa Taasisi ya Umma kusimamia mradi husika. 
Pia Dkt. Mhilu aliitaja miradi ambayo iko katika hatua mbalimbali za ubia kuwa ni mradi wa mabasi ya haraka Dar es Salaam (DART), mradi wa kufua umeme wa Kinyerezi III (TANESCO), mradi wa barabara ya tozo wa  Dar – chalinze (TANROADS), mradi wa uzalishaji wa madawa muhimu (MSD) pia iko miradi ambayo imechambuliwa na kutolewa taarifa zake kwa ajili ya kuboreshwa.
Dkt. Mhilu amesema kuwa utaratibu wa ubia sasa utakuwa kwenye ofisi moja ambayo ni Wizara ya Fedha na Mipango ili kuweka ufanisi katika utekelezaji wake ikiwa ni maamuzi ambayo yamefanyika katika awamu ya Tano ya Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Miradi ya ubia ni mkombozi katika kuboresha Bajeti ya Serikali na kuharakisha maendeleo endapo tu fursa za uwekezaji zitabuniwa vizuri, miradi itaandaliwa vizuri na taarifa sahihi zitatumika katika kuandaa miradi, wawekezaji wapatikane  kwa njia ya haki, uwazi na ushindani pamoja na mwekezaji kusimamiwa vyema katika ujenzi, uendeshaji na urejeshaji wa miundombinu.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.