Na Is-haka Omar, Zanzibar.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimemtumia salamu za rambi rambi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein kufuatia kifo cha Aliyekuwa Rais Mstaafu wa Zanzibar wa awamu ya pili na Makamo wa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Alhaji Mzee Aboud Jumbe Mwinyi kilichotokea Juzi Agost 14, Nyumbani kwake Dar es saalam.
Akitoa salamu hizo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai alisema kuwa CCM Zanzibar imepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha kiongozi huyo aliyetumikia taifa kwa uadilifu mkubwa na kuongoza harakati mbali mbali za ukombozi ndani na nje ya Tamzania.
Mh. Aboud Jumbe aliwahi kushika nyadhifa mbali mbali zikiwemo Rais wa Zanzibar wa awamu ya pili na Makamo wa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1974-1984.
Kufuatia kifo hicho Naibu Katibu Mkuu huyo Vuai alieleza kwamba Taifa limempoteza kiongozi muhimu aliyejitolea kupigania uhuru, haki na usawa na maendeleo ya wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika vipindi mbali mbali vya uongozi wake ndani ya chama na serikali.
Alisema CCM Zanzibar itaendelea kuenzi juhudi na falsafa za marehemu Jumbe hasa katika kupigania maslahi ya chama chake bila ya kujali vikwazo na changamoto zilizojitokeza katika enzi za utawala wake.
“Tumeshutushwa sana na kifo cha Mzee wetu ambaye alikuwa ni nguzo na mfano wa kuigwa kwa hakika taifa letu limempoteza mtu muhimu ambaye kwa kipindi cha uongozi wake alikuwa ni kiongozi muadilifu.
Lakini pia hatuwezi kuizungumzia historia halisi ya vyama vya ukombozi ndani ya taifa letu vikiwemo African association ilipoungana na Shiraz party na baadae kuzaa A.S.P ambapo waliungana na TANU na mnamo mwaka 1977 kuzaliwa CCM bila ya kumtaja Alhaji Aboud Jumbe aliyesimamia harakati hizo na kupatikana chama kimoja kilichokuwa na sera na misingi imara ya kuleta maendeleo ya nchi bila ya ubaguzi”, alifafanua Vuai.
Vuai alisema kwa niaba ya CCM Zanzibar anapenda kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki na wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kwa kufikwa na msiba huo.
Aidha aliahidi na kueleza kuwa Chama hicho kitaendelea kushirikiana na familia ya marehemu mara na baada ya msiba huo kwa lengo la kuthamini mchango wa Mzee Jumbe aliotumikia taifa kwa muda mrefu.
Aboud Jumbe alizaliwa Juni 14, 1920 Mkamasini, Unguja. Alishika madaraka ya kuiongoza Zanzibar mwaka 1972 baada ya kifo cha Mzee Abeid Amani Karume, kilichotokana kwa kupigwa risasi siku ya Aprili 7, 1972 Makao Makuu ya Afro Shirazi Party (sasa ofisi kuu ya CCM) Kisiwandui, Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu Vuai amemuombea marehemu Aboud Jumbe apumzike kwa Amani mahali pema peponi amen, na kusema inna Lilahi wa inna ilalhi raj’un.
No comments:
Post a Comment