Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu akiwahutubia
madiwani wa Wilaya ya ikungi ikiwa ni mara yake ya mwanzo tangu alipochaguliwa
na Rais John Magufuli kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo.
Kutoka
Kushoto ni Eng Sadick Chakka Mhandisi
wa Maji Wilaya ya Ikungi, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji jumanne Mtaturu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Wilaya ya Ikungi Rustika Turuka,
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ally J. Mwanga, na Kulia ni Abel
Suri Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Na
Mathias Canal, Singida
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu amewaonya baadhi
ya wanasiasa hususani madiwani katika Wilaya hiyo kupitia matamko yao ya kuzuia
ukusanyaji wa ushuru au kupiga vita vizuizi vilivyowekwa katika kata zote.
Madiwani hao wanatumia vibaya Uelewa
mdogo wa wananchi kwa kuwazuia kuchangia shughuli za maendeleo na ulipaji kodi
hivyo amewaagiza madiwani wote kuacha kuwatumia wananchi kwa muktadha wa
kuwanyima ufahamu bali wawe mstari wa mbele kuwaelimisha kwa kushirikiana na
wataalamu wanaopita kukusanya kodi
katika maeneo yao.
Dc
Mtaturu ameyasema hayo wakati wa kikao chake cha
kwanza cha Baraza la madiwani la Wilaya hiyo tangu alipoteuliwa na Rais John Magufuli kushiriki kwenye
baraza la madiwani ambapo pamoja na hotuba yake hiyo amewapongeza madiwani wote
kwa kuaminiwa na kuchaguliwa kwa ajili ya kuwawakilisha wananchi katika kata
zao.
Dc
Mtaturu amesema kuwa Baraza la madiwani ndio injini kuu ya maendeleo ya Wilaya, hivyo
kama kukiwa na Baraza lisilotimiza wajibu wake kamwe Wilaya haiwezi kutoka kwenye
kadhia iliyopo hususani katika sekta ya Kilimo, Mifugo, uvuvi, elimu, afya na
miundombinu.
“Wilaya
yetu bado ina changamoto nyingi sana, Natambua Wananchi wengi bado ni masikini kama sio wenye
kipato cha chini sana, Natambua Wananchi wengi wanajishughulisha na Kilimo na
Ufugaji ingawa wapo Wachimbaji wadogo wa Madini na Wafanyabiashara pia lakini natambua
huduma za jamii pamoja na miundombinu ni changamoto kubwa sana”
“Tumekuwa
Wilaya ya kuomba chakula cha msaada kila mwaka, maambukizi ya Virusi vya Ukimwi
VVU yanazidi kupanda, Elimu inazidi kushuka, mapato ya Halmashauri yameshuka,
wananchi wetu wamekuwa wakifuga na kulima kilimo kile kile cha mazoea, huduma
ya maji safi na salama imeendelea kuwa changamoto kwetu, Vituo vya Afya na Zahanati
havitoshelezi mahitaji” Alisema Mtaturu
Kwenye Huduma ya Afya katika Vijiji 101 vilivyopo
Wilayani Ikungi kuna Zahanati 34, Vituo vya Afya 3 na Hospitali 2, kwa uwiano
huu zisipofanyika jitihada zaidi hali ya wananchi itakuwa mbaya zaidi.
Hivyo Mkuu huyo wa Wilaya hiyo alisema kuwa Madiwani
wote wanatakiwa kuwa na mpango mkakati wa kuhakikisha huduma za Afya zinapatikana
kirahisi.
Katika hotuba yake Dc Mtaturu ameeleza kuwa Ni lazima kwenye Kamati za Maendeleo za
Kata (WDC) kuanzishwe mipango ya kuhakikisha kunapunguzwa Vifo vya Wakinamama
Wajawazito na Watoto kwa kuweka mikakati itakayohakikisha Wananchi wote hawaendi
umbali mrefu kutafuta huduma za Afya.
“Katika
suala hili la Afya ningependa kuzungumzia mabadiliko katika Sekta ya Afya
yanayoendelea hapa Nchini katika utoaji wa huduma. Mabadiliko haya yana lengo la kuinua kiwango cha ubora wa huduma za afya
zinazotolewa kwa wananchi na kuongeza kiwango cha uwajibikaji kwa wasimamizi na
watoaji wa huduma hizo. Ili kufanikisha
lengo hilo, madaraka, majukumu na kazi, rasilimali zaidi za afya zinahitajika
kwa kuitaka jamii kuchangia katika mifuko ya Afya ya Jamii (CHF)” Alisema Mtaturu
Katika Mfuko wa
Afya (CHF) Kaya moja itatakiwa kuchangia Tsh. 10,000/= na atatibiwa
Baba, Mama na Watoto wanne kwa mwaka mzima, hivyo Mwananchi akiuza kuku mmoja
tu anatosha kumtibia yeye mwenyewe na familia yake kwa mwaka mzima.
Mwananchi
asipojiunga na huduma hii atatakiwa kutoa Papo kwa Papo Tsh. 7,000/= pale anapougua hii elfu
saba ni ya kumuona Daktari bila dawa, Mwananchi huyu akiuguliwa na watu watano,
itamlazimu kutoa Tsh. 35,000/= kwa hiyo Mwananchi ambaye hajajiunga na CHF
atapata hasara ya Tsh. 25,000/= na wakati mwingine anaweza akauguliwa akiwa hana hata hela ya kutibiana hatimaye anahatarisha
maisha ya watu wake wa karibu.
Dc
Mtaturu amewataka Viongozi hao kujitafakari kwa
nini waliomba ridhaa ya kuwaongoza Wananchi wa Ikungi, kama waliomba nafasi
hiyo kwa ajili ya kuwatumikia Wananchi lakini kwenye Kata zao Shule za
Sekondari hazina Maabara, hakuna Zahanati na Kituo cha Afya, hakuna barabara,
hakuna huduma ya maji safi na salama na hakuna Shule; Wanafunzi wanatembea umbali
mrefu kufuata Shule na hawana mpango wowote ule wa kusogeza karibu huduma hizi basi
wanatakiwa kujitafakari upya.
Mkuu huyo wa Wilaya ameahidi kushirikiana na kila Kiongozi
bila kujali itikadi ya Chama chake, Dini yake au rangi yake katika kuwaletea
maendeleo Wananchi wa Ikungi.
Akitoa
salamu za shukrani kwa niaba ya Madiwani wote kwa hotuba ya Mkuu wa Wilaya ya
Ikungi, Mwenyekiti wa kamati ya huduma za jamii ambaye ni Diwani wa Kata ya
Issuna Steven Misai amesema kuwa Hotuba ya Mkuu huyo inaonyesha taswira
mpya ya kuinusuru Wilaya hiyo katika sekta ya elimu, afya, na miundombinu.
Missai
alisema kuwa maagizo ya hotuba yake yatafanyiwa kazi na madiwani wote ili
kuifanya wilaya ya Ikungi kuwa nguzo katika sekta hizo hususani ujenzi wa maabara.




No comments:
Post a Comment