Habari za Punde

*SUMATRA KUENDELEA KUKUSANYA MAONI YA WADAU.

Na Abushehe Nondo, MAELEZO.
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa  Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imesema kuwa bado inaendelea kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wa usafiri wa treni inayofanya safari zake kati ya Stesheni na Pugu jijini Dar es Salaam.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja Mawasiliano wa SUMATRA, Bw. David Mziray ambaye alibainisha kuwa kwa sasa bado wanaendela kupokea maoni kutoka kwa wadau kama sheria ya mamlaka hiyo inavyoelekeza kabla ya kuja na kiwango rasmi cha nauli ya usafiri huo.
“Tumetoa muda mpaka Agosti 19 mwaka huu iwe ndio mwisho wa kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusiana na bei elekezi ya nauli kwa treni inayofanya safari zake kati ya Stesheni na Pugu” Alisema Mziray.
Pia, Mziray alifafanua kuwa kwa kipindi hiki ambacho wanapokea maoni wameielekeza Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) waendelee kutoza nauli ya shilingi 400 kwa watu wazima na shilingi 200 kwa watoto na wanafunzi mpaka hapo itakapoamuliwa vinginevyo.
Alieleza kuwa tangu usafiri huo wa treni uanze huduma zake imeonekana kuwapunguzia wananchi adha ya kusafiri muda mrefu njiani na sasa wanaweza kuwahi katika maeneo yao ya kazi na biashara wakiwemo wanaokwenda kwenye soko la Kimataifa la samaki la Ferry.
Aidha, aliongeza kuwa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo ya usafiri pasipo na matatizo yoyote kampuni ya Reli Tanzania (TRL) inatarajia kuongeza mabehewa kutoka 15 yaliyopo sasa hadi kufikia mabehewa 20.
Akizungumzia baadhi ya changamoto walizoziona tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo ya usafiri wa Treni alisema kuwa ni pamoja na ukosefu wa huduma ya vyoo na maji katika baadhi ya vituo.
“Tunatarajia hivi karibuni Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) itajenga vituo vipya na kufanya ukarabati kwenye vituo vya zamani ili kuweza kuwaondolea usumbufu wananchi kwa kuweka huduma mbalimbali ikiwemo vyoo na maji kwenye vituo hivyo” Alisema Mziray.
Treni ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) inayofanya safari zake kati ya Stesheni na Pugu ilizinduliwa hivi karibuni na Waziri wa Ujenzi ,Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa na imekuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam hasa wakazi wa maeneo ya  Gongolamboto, Pugu na Chanika.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.