Habari za Punde

*TANZANIA KUWA MWENYEKITI KAMATI YA TROIKA

Na. Immaculate Makilika na Abushehe Nondo- MAELEZO
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga amesema Tanzania imepokea nafasi ya Uenyekiti wa Kamati ya TROIKA ya Siasa na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) inayosimamia masuala ya Ulinzi na Usalama.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Balozi Mahiga alisema Tanzania imepata nafasi hiyo wakati wa Mkutano wa SADC uliojadili masula ya Ulinzi na Usalama uliofanyika hivi karibuni mjini Maputo, Msumbiji.
“Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli atapokea nafasi hiyo ya kuwa mwenyekiti wa TROIKA kutoka kwa Rais wa sasa wa Msumbiji, Filipe Nyusi, nafasi inayodumu kwa kipindi cha mwaka mmoja” alisema Balozi Mahiga.

Aliongeza kuwa Mkutano huo wa TROIKA unatarajiwa kufanyika Agosti 29 na 30 mwaka huu huko Mbabane nchini Swaziland.
Aidha, Balozi Mahiga alisema kuwa SADC ni jumuiya iliyopiga hatua katika kusimamia masuala ya ulinzi, usalama na diplomasia jambo ambalo haliko katika jumuiya ya Afrika Mashariki hivyo kusaidia kutatua masuala yanayohusu hali tete za usalama katika ukanda huo.
Kwa mujibu wa Waziri Mahiga alisema mkutano wa TROIKA ni sehemu ya maandalizi ya kikao cha wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika kinachotarajiwa kufanyika baadae mwezi huu ambapo, taarifa ya hali tete ya usalama ya nchini Lesotho itatolewa.
Waziri Mahiga, alisema katika mkutano wa SADC uliofanyika mapema mwezi huu Maputo Msumbiji uliitaka nchi ya Lesotho kutekeleza masuala kadhaa katika kutafuta suluhu ya matatizo nchini humo, ikiwemo kufanya mageuzi ya katiba, mageuzi ya sekta ya ulinzi na usalama pamoja na kufanya marekebisho katika sekta ya utawala.
Mkutano huo wa SADC, vilevile unatarajiwa kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili jumuiya hiyo ikiwemo mgogoro wa kisiasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kufuatia kuibuka kwa makundi mbalimbali yanayohatarisha amani mashariki mwa nchi hiyo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.