Habari za Punde

*TRA YASISITIZA MISAADA HUWA HAITOZWI KODI

Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa ufafanuzi juu ya utozwaji wa kodi za misaada inayotolewa na wadhamini kusaidia Sekta ya Maendeleo ya Michezo Nchini.

Ufafanuzi huo umetolewa leo na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi, Richard Kayombo kutokana na habari iliyochapishwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari kuhusu Serikali kukosa mabilioni ya fedha kwa sababu ya kutokukusanya kodi ya fedha zinazotolewa na wadhamini kwenda kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

“Fedha zinazotolewa kama msaada kutoka kwa wadhamini huwa hazikatwi kodi lakini TRA hupata mapato yake kutokana na matumizi ya fedha hizo hasa pale wahusika wanapozitumia katika shughuli za kiuchumi”,alisema Kayombo.

Kayombo ametaja baadhi ya shughuli za kiuchumi zinazoweza kuwaingizia mapato kutoka kwenye misaada hiyo kuwa ni; kodi za waajiriwa wakiwemo makocha na wachezaji, makusanyo ya uwanjani ,kupewa huduma za kitaalam pamoja na majengo ya kupangisha au kupanga.

Amefafanua kuwa kama Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini  (TFF) linakodisha jengo basi fedha wanazopata lazima walipe kodi ya asilimia 10 kutoka kwenye fedha hizo na kama wao ndio wamekodi jengo kwa ajili ya matumizi yao wanatakiwa kutoa kodi ya asilimia 5.

Kwa upande wa kodi kutoka kwa waajiriwa, Mamlaka hiyo inaendelea kutoa elimu kwa vilabu vya michezo kuwa michezo ni ajira kama ajira zingine hivyo mishahara yao inatakiwa kukatwa kodi kulingana na kiasi wanacholipwa.

Zoezi la kuwatoza kodi makocha na wachezaji limeanza rasmi mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.