Na Ismail Ngayonga- MAELEZO, Dar es Salaam
KAMPUNI ya Reli Tanzania (TRL) inakusudia kuongeza mabehewa 4 kwa ajili ya abiria wanaotumia huduma ya usafiri wa treni kutoka kituo cha Dar es salaam hadi Pugu kufikia mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.
Ongezeko hilo litafanya mabehewa kufikia 20 kutoka 16 yaliyopo sasa hali itakayoongeza ufanisi wa utoaji wa huduma ya usafiri huo kwa abiria wanaotumia usafiri huo.
Hayo yamesemwa na Afisa Uhusiano wa TRL, Midladjy Maez ambaye alisema hatua hiyo ni mkakati wa TRL wa kukabiliana na changamoto ya usafiri huo kwa nyakati za asubuhi na jioni ambapo choombo hicho cha usafiri kimekuwa kikikabiliwa na ongezeko kubwa la watumiaji.
Maez alisema usafiri huo kwa sasa umekuwa ukitumiwa na idadi kubwa ya wananchi hususani kwa nyakati za asubuhi na jioni na hivyo kusababisha kuzidiwa na wasafiri ikilinganisha na uwezo wa chombo hicho.
“Nawaomba abiria wote wafuate taratibu wakati wa kutumia usafiri wetu ikiwemo kukata tiketi katika vituo vyetu, kwani iwapo itabainika abairia hana tiketi na akaingia ndani ya treni basi adhabu kali zitachuliwa dhidi yake ikiwemo kifungo cha miezi 3 hadi 6” alisema Maez.
Aidha Maez aliwataka abiria kutumia lugha za kistaarabu kwa wafanykazi wa treni pindi wanapobaini changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza wakati wa kutumia vyombo hivyo badala ya kutumia lugha zisizo za ustaarabu ambazo huwakwaza watumishi wa treni hiyo.
Akizungumzia kuhusu mabadiliko ya matumizi ya kituo cha Kamata kilichopo katika eneo la karikoo Jijini Dar es Salaam, Maez aliwataka abiria wanaotumia kituo hicho kuhamia katika kituo kidogo kilichopo ndani ya ofisi za TRL Mtaa wa Nkhurumah ambapo abiria wote watahudumiwa pasipo na usumbufu.
Akifafanua zaidi Maez alisema ni wajibu wa abiria wote kufuata sheria, kanuni na taratibu za matumizi ya chombo hicho ikiwemo kukata tiketi kwani utaratibu huo hutumika ulimwenguni kote na si Tanzania pekee.
No comments:
Post a Comment