Na Georgia Misama – MAELEZO
Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) imejipanga kutoa huduma bora kwa mashirika na taasisi zinazotarajia kuhamia Mjini Dodoma.
Hayo yamesemwa na Meneja Uhusiano TTCL Bw. Nicodemus Thom Mushi leo Jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya mpango wa miaka mitatu wa mageuzi ya kibiashara wa Kampuni hiyo.
Mushi ameeleza kuwa, katika mpango huo TTCL imejipanga vyema kufanikisha azma ya Serikali ya kuhamia mjini Dodoma kwa kutoa huduma bora kwani tayari kampuni hiyo ina rasilimali watu, vifaa na wataalamu wa kutosha katika kutoa huduma za Mawasiliano.
“Nitumie fursa hii kuwaomba taasisi zote za Umma zinazohamia Dodoma na Taasisi zote kwa ujumla kutumia huduma za TTCL ambazo zote zimethibitika kuwa ni huduma bora na za uhakika na zenye gharama nafuu,” amefafanua Mushi.
Aidha, kampuni hiyo imeboresha njia ya kusikiliza wateja ambapo hivi sasa malalamiko ya wateja hushughulikiwa ndani ya masaa matatu toka mteja anapotoa taarifa katika kituo cha huduma kwa mteja.
Akiongelea juu ya maboresho, Mushi amesema kuwa, kampuni hiyo imeleta huduma mpya ya 4G LET ambayo inapelekea intaneti yenye kasi zaidi, vile vile imeboresha miundo mbinu ya mitandao ya simu na data na kuondoa mitambo chakavu.
Sambamba na hayo Mushi amewahakikishia wateja kuwa TTCL ni kampuni pekee ambayo ni suluhisho la huduma bora na ya uhakika wakati wote na mahali popote iwe ni nyumbani, sehemu ya kazi na hata kwenye vyombo vya usafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
No comments:
Post a Comment