Habari za Punde

TFF WAOMBA KUJIRIDHISHA KUUPITIA MKATABA WA YANGA NA YANGA YETU, WAZEE,WANACHAMA WAOMBA KUTINGA KWA JPM

Na Ripota Wetu, Dar
SHIRIKISHO la Mpira Wa Miguu Tanzania (TFF) leo limefunguka kuhusu mchakato wa klabu ya Yanga kukodishwa kwa kampuni ya Yanga Yetu inayomilikiwa na Mwenyekiti wa Klabu hiyo Yusuf Manji.

Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa amezungumza kuhusu mabadiliko ambayo wameyafanya na kusema wao kama TFF bado hawajayatambua mabadiliko hayo na kwamba tayari wamemwandikia barua Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit ya kumtaka aonyeshe mkataba ambao wameingia na kampuni ya Yanga Yetu.

Mwesigwa amesama kuwa amemuandikia barua Katibu Mkuu wa Yanga ili awapatie nakala ya mkataba ule wa Yanga na Kampuni ya Yanga Yetu ili kama kuna jambo halijakaa sawa liweze kurekebishwa.

“Tungependa mkataba uwe wazi ili hata klabu zingine zijifunze, kwa hiyo Yanga tumewaomba walete copy ya huo mkataba ili tujiridhishe nini kinaazimwa na kipi kinauzwa, klabu itaendeshwaje na baada ya hapo kamati za TFF zitakaa kulijadili jambo hilo, kama itakuwa tofauti na kanuni zetu tutarudi kwao warekebishe mambo ambayo hayapo sawa,” alisema Mwesigwa.

Aidha Mwesigwa alisema kuwa uendeshwaji wa Klabu ni lazima ubadilike kuendana na wakati lakini hatutakiwi mabadiliko hayo ndiyo iwe chanzo cha kusababisha mvurugano ambao haukuwepo kwa muda mrefu.

''Mpaka sasa tumeshapokea barua nyingi za wanachama wa Yanga na baadhi ya wazee wa Yanga ambao wamekuja kwetu kuomba msaada ili tuwasaidie kulifikisha jambo hili kwa mkuu wa nchi''. alisema Mwesigwa

Aidha amesema TFF bado inatambua Yanga inasimamiwa na uongozi wa klabu kama ilivyokuwa awali ikiongozwa na Mwenyekiti, Yusuf Manji na kama kutakuwa na jambo la tofauti watatoa taarifa baada ya kujiridhisha na mfumo ambao Yanga itakuwa inautumia kukodisha timu kwa Kampuni ya Yanga Yetu.

1 comment:

  1. Wauza jezi wansina Sikh zao zinazidi kuyeyuka. Kwa mkuu wa nchi wakafanye nn wapiga dili hao kama wanahoja tar.23 waende mkutanoni

    ReplyDelete

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.