Na: Jovina Bujulu –
MAELEZO
Mizigo mikubwa
waliyonayo wanawake ni miongoni mwa changamoto za kijamii ambazo zimekuwa
kikwazo kwa wao kushiriki kikamilifu katika masuala ya siasa.
Hayo yamesemwa na
Balozi Getrude Mongella ambaye pia ni Rais Mstaafu wa Bunge la Afrika alipokuwa
akizungumzia ushiriki wa wanawake katika siasa nchini.
“Changamoto kubwa ni
pamoja na teknolojia duni ambayo inamlazimisha mwanamke kuendelea kulima kwa
kutumia jembe la mkono, kutembea umbali mrefu kutafuta maji, kutafuta kuni na
suala zima la kulea watoto” alisema Balozi Mongella.

Akizungumzia suala la
teknolojia duni alisema kuwa katika nchi zinazoendelea hilo limeendelea kuwa
tatizo kubwa na kwa kuwa wanawake ndio wazalishaji mali wakubwa, wamejikuta
wanaweka nguvu zao nyingi katika matumizi ya jembe la mkono. Hivyo ukulima kwa
kutumia jembe la mkono haukidhi mahitaji yao ya chakula katika familia na
kujikuta wamebaki kuwa omba omba.
Pamoja na changamoto
hizo Balozi Mongella amesema kuwa ushiriki wa wanawake bado ni mkubwa na
ameitaka jamii kuwawezesha kubeba baadhi ya mizigo kwa mfano kuimarisha huduma
za afya ya jamii.
Balozi Mongella alitoa
ushauri kwa jamii kutokukaa kimya bali kuzungumzia changamoto hizo na utatuzi
wake ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha wanaume, kwani wakielimika na kutumika
vizuri baadhi ya changamoto zitaondoka na kasi ya mwanamke kupiga hatua itakuwa
kubwa.
Aidha, alivitaka
vyama vya wanawake kuamka na kuendeleza mapambano ya kumkomboa mwanamke kwani
ajenda ya wanawake ni ya kudumu na
haijakamilika hata kidogo.
Zaidi ya hayo, Balozi
Mongella amewataka wanawake kutambua nafasi yao katika kuchangia uchumi wa
taifa, ili wafike mahali waonyeshe mchango wao katika Tanzania ya viwanda ambayo
Watanzania wanaitaka na kuwashauri wanawake waliopata elimu kusaidia kuwavusha wanawake
wengine.
Naye Mwenyekiti wa Chama
cha ACT-Wazalendo ambaye alikuwa Mgombea Urais pekee mwanamke katika uchaguzi
uliopita wa 2015, Mama Anna Mgwira alisema wanawake wakipewa nafasi wanajitoa
kwa ukamilifu hivyo aliwataka wasimamie nafasi zao huku wakifanya kazi kwa
weledi, uaminifu, wajiheshimu na wawajibike ili kuondokana na dhana ya kwamba
hawawezi kazi bila kusimamiwa na kusaidiwa


No comments:
Post a Comment