Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imepitia ripoti za michezo yote ya Ligi Kuu Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na Ligi Daraja Pili (SDL) na kufanya uamuzi ufuatao.
Mechi namba 54 (Simba 4 v Njombe Mji 0).
Klabu ya Simba imepewa Onyo Kali kutokana na Kocha wake Msaidizi Masoud Djuma kuanza kufundisha bila kuwa na vibali vya kuishi na kufanya kazi nchini. Uamuzi huo umefanywa kwa kuzingatia Kanuni ya 40(13) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Makocha.
Pia klabu hiyo imetakiwa kufikia Novemba 10 iwe imewasilisha Bodi ya Ligi nakala ya vibali hivyo, na kukumbushwa kuwa mahitaji ya nyaraka hizo ni kwa mujibu wa Kanuni za Ligi, lakini pia sheria za nchi.
Vilevile klabu ya Simba imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa timu yake kuwasilisha orodha ya wachezaji wake (team match list) nje ya muda wa kikanuni. Kitendo cha timu hiyo ni kukiuka Kanuni ya 14(2k) ya Ligi Kuu. Adhabu dhidi yao imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu.
Klabu ya Njombe Mji imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na kuonesha vitendo vinavyoashiria imani za ushirikina katika mechi hiyo wakati ikiwasili uwanjani. Adhabu dhidi ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Mechi namba 56 (Stand United 0 v Yanga 4). Klabu ya Stand United imetozwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kutokana na golikipa wao kuvaa jezi yenye namba tofauti na ile iliyosajiliwa, kitendo ambacho ni ukiukaji wa Kanuni ya 60(11) ya Ligi Kuu kuhusu Usajili. Adhabu dhidi yao imezingatia Kanuni ya 60(12) ya Ligi Kuu.
Mechi namba 57 (Azam FC 1 v Mbeya City 0). Mwamuzi Shakaile Ole Yanga Lai amefungiwa miezi mitatu kwa kutoripoti na kuchukua hatua dhidi ya kitendo cha Kipa Owen Chaima wa Mbeya City kumpiga kofi mshambuliaji wa Azam FC. Kitendo cha Mwamuzi huyo ni ukiukaji wa Kanuni ya 38(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Waamuzi wakati adhabu dhidi yake imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 38(5) ya Ligi Kuu.
Naye Kamishna wa mechi hiyo, David Lugenge amefungiwa miezi mitatu kwa kushindwa kuripoti tukio hilo. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 39 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Kamishna.
Mechi namba 58 (Yanga 1 v Simba 1). Klabu ya Yanga imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na mashabiki wake kurusha uwanjani chupa zinazosadikiwa kuwa na mikojo. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 42(1) kuhusu Udhibiti wa Klabu.
No comments:
Post a Comment