Habari za Punde

MSANII LULU AHUKUMIWA MIAKA MIWILI JELA KIFO CHA KANUMBA

 Msanii wa Filamu nchini, Elizabeth Michael 'Lulu', akiwasili katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, leo asubuhi kabla ya kusomewa hukumu yake ya kwenda Jela miaka miwili  kwa kosa la kumuua bila kukusudia aliyekuwa mpenzi wake msanii wa Filamu, Steven Kanumba. 
***********************************
Na Furaha Omary, Dar
MSANII wa filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu ‘Lulu’, amehukumiwa kifungo cha miaka miwili Jela baada ya mahakama kumtia hatiani kwa kosa la kumuua bila kukusudia aliyekuwa mpenzi wake na msanii nguli wa filamu nchini, Steven Kanumba.
Hukumu hiyo iliyoibua vilio Mahakamani hapo kutoka kwa ndugu wa Lulu akiwemo mama yake Lucresia Karugila,  wasanii wenzake ndugu jamaa na marafiki pamoja na  mama wa marehemu Kanumba Flora Mtegoa,    iliyotolewa leo mchana katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Lulu ambaye alifika mahakamani hapo mapema asubuhi akitokea nyumbani akiwa amevalia dera huku akifunga kitambaa cha dera hilo kichwani akiambatana na ndugu wa familia yake na kuingia katika ukumbi wa wazi ambako Jaji Sam Rumanyika aliketi kusoma hukumu mbalimbali ikiwemo hukumu yake.
Katika ukumbi huo, uliokuwa umefurika umati wa watu, Jaji Rumanyika alianza kusoma hukumu za washitakiwa wengine na ilipotimu saa 4.16 asubuhi, aliitwa mshitakiwa Lulu ili aweze kupanda kizimbani ili kusomewa hukumu yake.
Jaji Rumanyika alianza kusoma hukumu hiyo kwa kueleza kuwa Lulu alifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Aprili 12, 2012 ambako alikuwa akishitakiwa kwa kosa la kumuua Kanumba alilokuwa akidaiwa kulitenda Aprili 7, 2012, maeneo ya Sinza Vatican, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.
Alisema wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, upande wa jamhuri ulikuwa ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Faraja George akishirikiana na Wakili Yussuf Abdul huku Lulu akitetewa na Wakili Peter Kibatala. Alisema kwa upande wa mahakama aliketi yeye na wazee watatu wa baraza.
Jaji Rumanyika alisema upande wa jamhuri, ulileta mashahidi wanne na mshitakiwa Lulu alijitetea mwenyewe na hakuwa na shahidi zaidi ya mahakama kupokea maelezo kama kielelezo cha upande wa utetezi ya Josephine Mushumbus.
 Lulu akiwa na huzuni baada ya kusomewa hukumu yake
******************************************
KESI YA UPANDE WA JAMHURI
Jaji Rumanyika alisema kesi ya upande wa jamhuri imejikita balabala katika ushahidi wa mazingira na hakukuwepo hata chembe ya ushahidi wa moja kwa moja. KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA

“Ushahidi wa mazingira, hata mshitakiwa alikubali kwamba alikuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu Kanumba ambaye alikuwa mpenzi wake kwa kipindi kifupi cha miezi minne kuanzia Januari hadi umauti ulipomkuta Aprili,” alisema Jaji Rumanyika.
Alisema kwa msimamo wa Mahakama ya Afrika Mashariki na Mahakama ya Rufani Tanzania, katika ushahidi huo wa mazingira, mshitakiwa anatakiwa kutoa maelezo yanayojitosheleza juu ya maswahibu gani yalimkuta marehemu.
Jaji alisema msingi pekee wa kumtia hatiani kwa ushahidi wa mazingira ni pale ambapo kama ushahidi huo utamnyooshea kidole mshitakiwa mwanzo hadi mwisho.
MAELEZO YA LULU KAMA YANAKIDHI VIGEZO
Jaji Rumanyika alianza kwa kuchambua kwamba, shahidi wa kwanza wa upande wa jamhuri aliyasema yote aliyoyasema ambayo hata Lulu alikubali kuwa mtu wa mwisho na marehemu Kanumba.
“Ilianza  kama mzozo hatimaye mshitakiwa alianza kupigwa na marehemu Kanumba, utasema kupigwa au mzozo. Kwa mujibu wa Kamusi kugombana inatafsiriwa kama patashika iwe ya mzozo au maneno mmoja akikabiliana na hali hiyo,” alisema Jaji Rumanyika na kuongeza kuwa:
“Kwa maoni yangu, kuanguka au kudondoka kwa mmoja kati ya hao ni yanayotazamiwa mmoja kumsukuma au kumkaba,” alisema.
Jaji Rumanyika alisema mshitakiwa Lulu alisema katika utetezi wake, ushahidi wake akionesha marehemu Kanumba alilewa kama inavyojulikana walevi mambo wanayoyafanya ni kuanguka.
“Katika hali hii mshitakiwa alitakiwa kutoa maelezo yanayojitosheleza, alijikanganya katika ile hali ya ulevi marehemu alimfukuza, akamkamata kama hatua 27 na kumburuza na kumrudisha chumbani. Mshitakiwa Lulu hakuwahi kusema Kanumba alikuwa akianguka anguka,” alisema Jaji Rumanyika.
 Mama mzazi wa Lulu, Lucresia Karugila  (katika), akitoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, huku akishikiliwa na nduguze baada ya mtoto wake Elizabeth Michael 'Lulu', kuhukumiwa kwenda Jela miaka miwili kwa kosa la kumuua bila kukusudia Steven Kanumba. 
********************************************
JAJI: Maelezo ya Josephine hayakuwa na hadhi
Kuhusu maelezo ya Josephine Mushumbus ambaye alieleza Kanumba alikuwa mteha wake kwenye kituo chake cha tiba mbadala ambayo yaliletwa na upande wa Lulu, Jaji Rumanyika alisema labda maelezo hayo ambayo ni kielelezo cha pili cha utetezi yawe yameungwa mkono na chanzo kingine lakini hakuna kilichounga mkono, hivyo kinaacha mamilioni ya mashaka.
“Maelezo hayo siyo cheti cha daktari, hayakuwa wala na hadhi ya kuwa cheti cha daktari. Katika kesi hii kongwe miongoni mwa kesi kongwe, daktari Pankrasi ambaye ni shahidi wa pili wa upande wa jamhuri, alijinadi alikuwa daktari wa familia ya Kanumba, sikuambiwa wala mahakama haikuambiwa Josephine Mushumbus alikuwa daktari wa familia,” alisema Jaji Rumanyika.
Jaji Rumanyika alisema daktari Pankrasi alitegemewa atuambie historia ya marehemu Kanumba kama Josephine alivyofanya.
“Daktari pekee wa familia tuliyebaki naye ni Pankrasi ambaye alitakiwa atuambie historia ya marehemu. Hata mshitakiwa ambaye ni mpenzi wa miezi minne wa Kanumba hakutuambia historia hiyo hadi tulipoipata kwa Josephine,” alisema Jaji Rumanyika.
Aliongeza kuwa : “Ninakinzana na kwa hekima hata pale marehemu alipotaka kumpiga kwa panga, mshitakiwa hakujaribu kumpiga hata kwa kumsukuma, kama kwamba mshitakiwa alichukua utaratibu wa Kibiblia kwamba akikupiga shavu la kushoto geuza na la kulia.”
Jaji Rumanyika alisema mtu wa mwisho kuwa na marehemu ni mshitakiwa,  jambo ambalo alikubali, hakutoa maelezo ya kina na ya kujitosheleza nini kilitokea hatimaye marehemu alikutwa na umauti.
“Inabaki kwa watu wawili kueleza hilo ambao ni marehemu Kanumba na mshitakiwa Lulu. Mshitakiwa ndiye amebaki hata marehemu angefufuka ushahidi wake mahakama haiwezi kuuchukua,” alisema.
Mama mzazi wa Steven Kanumba, Flora Mtegoa, akitoka mahakamani hapo ameshikiliwa na nduguze.
*****************************************
JAJI; Lulu siyo watoto waliolengwa na Sheria ya Watoto
Jaji Rumanyika alisema kwamba pengine mwingine anaweza kueleza kwamba wakati tukio linatokea mshitakiwa ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 22, alikuwa na umri wa miaka 17, hivyo hakuwa mtu mzima, asingeweza kujua mabaya na mazuri.
Kuhusu hili kuna kanuni kuu, kwa maoni yangu ina tofauti zake kwa sababu tatu ambazo ni ya  kwanza, mshitakiwa alikuwa mtoto lakini kwa mujibu wa kielelezo cha pili cha upande wa jamhuri alikuwa anaitwa mke na mshitakiwa anakubali.
Jaji Rumanyika anataja sababu ya pili kwamba mshitakiwa ni yule mtoto  anayethibitisha kuamua hata ndivyo sivyo tofauti na maelekezo ya wazazi wake, alikuwa anaamua wapi aende, arudi saa ngapi afanye.
Alisema aina hiyo ya mshitakiwa huyo mtoto au wenzake wanaweza kuamua kutoka nyumbani hata usiku wa manane akamtembelea mpenzi wake ili akaendelee na mambo yake, mambo ambayo yote ameeleza mshitakiwa mwenyewe kwenye ushahidi wake.
“Baada ya kusema yote mshitakiwa siyo wale watoto waliolengwa na Sheria ya Watoto. Kwa maoni yangu kama mtoto kwa umri ameweza kufanya ya watu wazima akajiamini na kuyaweza kuyafanya, mahakama hii itegemee Mwenyezi Mungu atuepushie mbali kuona wazee wanaofanya mambo ya kitoto wakisubiri walengwe,” alisema.
Jaji Rumanyika alisema maana ya ukomavu siyo siku anazosheherekea, haya yanaonesha kukua na kuzeeka ni jambo moja lakini ukomavu jambo lingine.
Alisema hataki kuwa jaji wa kwanza kuonesha kushindwa  utawala wa sheria, kama mahakama itaacha kufanya yale ambayo sheria haijaruhusu kwa kuiangalia kwa upana wake
“Najiridhisha kifo cha Kanumba kilitokana na ugomvi ndiyo maana mshitakiwa Lulu ameshitakiwa kwa kosa la kumuua bila kukusudia. Nakubali katika mashauri ya mauaji nia ya muuaji siyo lazima idhibitike inatokana na saikolojia. Itoshe kwa sababu mshitakiwa alisema katika utetezi wake, marehemu alikuwa na wivu usiokuwa na mipaka usio wa msingi ulisababisha kupigwa.
“Hakuna mchezo usio na kanuni. Mshitakiwa aliamua kuingia katika mchezo huu, alitakiwa aingie kwenye kanuni, wivu wa maendeleo huzaa maendeleo na wivu wa mapenzi huzaa maangamizi. Mshitakiwa alifahamu tangu Januari hadi Aprili kwamba marehemu alikuwa na wivu uliovuka mipaka basi hata pale  marehemu alipomshuku kuongea na wapenzi wake alitakiwa aache lakini aliamua kama noma na iwe noma,” alisema.
“Mshitakiwa namtia hatiani kama alivyoshitakiwa,” alisema Jaji Rumanyika ambapo baada ya kumtia hatiani mshitakiwa hao kabla ya kutoa adhabu aliwasikiliza mawakili wa pande zote husika.
Kibatala amuombea Lulu kifungo cha nje, amebadilika.
Baada ya kutiwa hatiani mshitakiwa huyo, Wakili wa Serikali, Faraja alidai ni mkosaji wa mara ya kwanza na kuiomba mahakama itoe adhabu kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wa Wakili wa Lulu, Kibatala alidai Lulu ni mkosaji wa mara ya kwanza na kosa lilitendeka katika mazingira ya ugomvi na hakuna ushahidi kama alikusudia kilichotokea.
Wakili Kibatala alidai mshitakiwa amebadilika na kurudi katika mstari mnyoofu katika jamii, amejiunga na chuo ambapo ameshamaliza Diploma anasubiri kwenda ngazi nyingine.
Pia, alidai kiuchumi anajishughulisha na ubalozi wa taasisi mbalimbali na ataangaliwa kwa macho fulani na jamii inayomzunguka na ni sehemu ya fundisho, wapo watakaojitokeza na kujitolea kumrudisha katika mstari ulionyooka.
Kibatala alidai mahakama imemuona mshitakiwa alikuwa na uhuru ambao hauendani na mazingira ya kukaa na wazazi. Alidai wazazi wake hawaishi pamoja jambo ambalo lina madhara.
Wakili huyo alidai mshitakiwa huyo alishakaa mahabusu kwa miezi 10, kwa maoni yake ni adhabu kwa mazingira ya tukio hilo na anategemewa na mama yake na wadogo zake. Aliomba  mahakama imfikirie kumpa adhabu ya kifungo cha nje.
ADHABU YAANGUA VILIO
Ilipotimu saa 5.07 asubuhi, Jaji Rumanyika alianza kutoa adhabu ambapo akisema katika kutoa adhabu msingi ambao mahakama inapaswa kuuzingatia matakwa ya kanuni.
“Namhukumu mshitakiwa kifungo cha miaka miwili gerezani,” alisema Jaji Rumanyika.
Baada ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Lulu ambaye wakati hukumu hiyo ikisomwa alikuwa akionekana kuwa na wasiwasi kwa kufuta uso huku akishika dira lake mara kwa mara, alichukuliwa na askari waliokuwepo mahakamani hapo na kumpeleka mahabusu.
Wakati  msanii huyo akienda mahabusu kusubiri taratibu ili apelekwe gerezani kuanza maisha mapya, mama yake mzazi, Lucresia Karugila,  ndugu, jamaa na marafiki zake waliokuwepo kwenye viunga hivyo vya mahakama walishindwa kujizuia na kuanza kulia.
MAMA KANUMBA; HAKI IMETENDEKA
Baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo, mama wa marehemu Kanumba, Flora  ambaye alikuwa akihudhuria usikilizwaji wa shauri hilo tangu ulipoanza Oktoba 19, mwaka huu, alikuwa akilia hali iliyowafanya ndugu wawili kumshikilia huku na kule.
Akizungumza kwa uchungu nje ya ukumbi wa mahakama, Mama huyo alisema: “Namshukuru Mwenyezi Mungu, mahakama imetenda haki. Rest in peace Kanumba. Naenda makaburini sasa.”
KIBATALA; Tutakata rufani
Kwa upande wake, Wakili Kibatala alidai kwamba watakata rufani kupinga hukumu hiyo ambapo wakati utaratibu huo ukiendelea wataomba Lulu awe nje kwa dhamana. Lulu aliondoshwa mahakamani hapo kupelekwa gerezani kwa kutumia gari la polisi aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba  T 475 BNM.
KESI ILIPOANZA KUSIKILIZWA
Jaji Rumanyika aliketi kusikiliza shauri hilo kuanzia Oktoba 19 mwaka huu hadi  Oktoba 26, mwaka huu ambapo  upande wa jamhuri mashahidi wanne ambao ni mdogo wa Kanumba, Sethi Bocso, daktari Pakrasi Kangaila,  askari polisi wa Kitengo cha Upelelezi, Ester Zefania na daktari bingwa katika uchunguzi wa magonjwa ya binadamu na uchunguzi wa vifo vya mashaka, Innocent Mosha kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ambaye alifanyia uchunguzi mwili wa Kanumba.
Baada ya shahidi wa nne wa upande huo kumaliza kutoa ushahidi, Jaji Rumanyika alimuona Lulu ana kesi ya kujibu kama alivyoshitakiwa na kutakiwa kutoa utetezi wake.
Katika utetezi wake, Lulu aliieleza mahakama kwamba kwa namna yoyote hajasababisha kifo cha aliyekuwa msanii nguli wa filamu nchini, Kanumba ambaye pia alikuwa mpenzi wake.
Alidai Aprili 7, 2012, alienda nyumbani kwa Kanumba, maeneo ya Sinza Vatican, Dar es Salaam, kwa nia njema na pengine bila ya Kanumba kuanguka, yeye ndiye angekuwa marehemu.
Lulu alidai yeye angekuwa marehemu kwa sababu Kanumba alikuwa akimshambulia kwa silaha aina ya panga na kwa umbile lake dogo hakuwa na namna yoyote ya kujitetea ndiyo maana alikuwa akikimbia wakati wa shambulio hilo.
“Sijahusika kwa namna yoyote kwa kifo cha Kanumba. Siku ya tukio nilienda kwa nia njema kama siku zote, badala yake Kanumba alianza kunishambulia akinihisi nilikuwa naongea na simu na mwanaume mwingine, akadondoka ghafla sijajua kwa sababu gani,” alidai Lulu katika utetezi wake.
Baada ya msanii huyo kutoa utetezi huo, mawakili wake waliomba mahakama kupokea maelezo ya Josephine kama sehemu ya utetezi wao. Aliomba mahakama ipokee maelezo hayo kwa kuwa shahidi huyo ameshindwa kufika kwani yuko nje ya nchi.
Hata hivyo, upande wa jamhuri ulipinga maombi hayo kutolewa na mawakili wa utetezi badala yake yatolewe na askari aliyeyachukua. Mahakama hiyo ilikubaliana na pingamizi la jamhuri na kuamuru askari aliyechukua maelezo ya Josephine kuhusu tukio hilo afike mahakamani hapo.
Amri hiyo ya mahakama ilitekelezwa ambapo askari Nyangea alifika mahakamani hapo na kuyasoma maelezo hayo ya Josephine ambaye alieleza Kanumba alikuwa miongoni mwa wateja wake katika kituo chake cha tiba mbadala.
Baada ya upande wa utetezi kufunga ushahidi wao, Jaji Rumanyika alitaka kupata maoni kutoka kwa wazee wa baraza kama mshitakiwa huyo ana hatia ama la baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote husika.

Wazee hao wa baraza katika maoni yao waliieleza mahakama kwamba wameridhika na ushahidi wa upande wa jamhuri hivyo wanaona Lulu alimuua bila kukusudia Kanumba.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.