Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao (wa pili kushoto) akizungumza na wandishi wa habari leo. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Wanachama na Sheria, Edward Mwakingwe, Mkurugenzi wa Mashindano Efrem August na Mkurugenzi wa Masoko Aaron Nyanda
*************************************
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema litawachukulia hatua za kisheria watu ambao wataeneza na kusambaza habari ambazo hazina ukweli kuhusu shirikisho hilo.
Hayo yamesemwa leo na Kaimu Katibu Mkuu wa TFF Wilfred Kidao wakati akitoa ufafanuzi wa ujumbe/habari iliosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuongeza posho kwa wajumbe wa kamati ya utendaji pamoja na kuanzisha malipo ya mishahara kwa Rais na Makamu wake.
Kidao alisema viwango vya posho za vikao vya Kamati ya Utendaji havijawahi kujadiliwa wala kubadilishwa (kuongezwa) tangu uongozi mpya uingie madarakani bali kamati ilipitisha posho y ash. Milioni 1.5 kwa wajumbe kwa miezi mitatu ili iwasaidie kutekeleza majukumu yao.
“Wajumbe wa kamati ya utendaji wanawezeshwa kutekeleza majukumu yao kwenye kanda zao kwa kulipwa sh. Milioni 1.5 ambayo ni sawa na laki tano kila mwezi na hii posho anapewa baada ya kuwasilisha taarifa ya kazi ambazo amezifanyaka katika kipindi cha miezi mitatu kwenye kanda yake,” alisema Kidao.
Kidao alisema kuhusu mshahara wa Rais wa TFF na Makamu wake hilo halikufikiwa mwafaka kwani halikufuata taratibu japo wajumbe wa kamati ya utendaji walishauri ofisi ya Rais ihudumiwe na TFF kama ilivyo kwa ofisi za marais wa FIFA na CAF.
“Rais wa TFF Wallace Karia alikataa kwa kusema, anaamini sio wakati mwafaka wa yeye kuchukua posho hadi taasisi itakapokaa vizuri na taratibu zote kufuatwa na pia yeye ni mtumishi wa serikali hawezi kupokea mshahara miwili kwa wakati mmoja,” alisema Kidao.
Kidao ambaye katika mkutano huo alikuwa ameambatana na wakurugenzi wapya akiwemo Mkurugenzi wa Wanachama na Sheria, Edward Mwakingwe alimwagiza kuanza kufanya taratibu za kuwafikisha mahakama watu wote waliosambaza taarifa hiyo kwani ina lengo la kuichafua taasisi hiyo.
“Nakuagiza mwanasheria wa TFF, kufungua mashtaka kwa wale waliosambaza ujumbe kwenye mitandao ya kijamii wenye lengo la kuichafua taasisi hiyo kwani sheria ya mitandao inakataza kusambaza habari ambazo zinalengo la kuchafua na kuharibu twasira ya taasisi,” alisema Kidao.
Pia Kidao alisema ofisi yake ipo wazi muda wote endapo kuna habari wanataka kupata ufafanuzi wasisite kumpigia na endapo wataona simu haipokelewi watu ujumbe mfupi maana inawezekana akawa yupo kwenye kikao.
Katika kikao hicho aliwatambulisha wakurugenzi wapya ambao ajira zao zilipitishwa na kamati ya utendaji ambao ni Mkurugenzi wa Wanachama na Sheria, Edward Mwakingwe, Mkurugenzi wa Masoko Aaron Nyanda, Mkurugenzi wa Mashindano Efrem August na Mkaguzi wa ndani John Benjamin
No comments:
Post a Comment