MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetupilia mbali maombi ya upande wa mashtaka ya kupinga dhamana katika kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili aliyekuwa Rais Klabu ya Simba, Evans Aveva na mwenzake Godfrey Nyange.
Akisoma uamuzi huo leo mahakamani hapo, Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba, amesema kitendo cha upande wa mashtaka kukata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania ya kupinga dhamana haizuii washtakiwa kupata dhamana, hivyo maombi yanatupiliwa mbali.
" Kukata rufaa haiondoi maamuzi ya mahakama hii ambayo imetoa, hivyo wakati washtakiwa watakapokuwa nje kwa dhamana na rufaa itaendelea kusikilizwa," alisema.
Baada ya uamuzi huo, Wakili wa Serikali Mkuu, Shadrack Kimaro, alidai hajalizishwa na uamuzi huo, hivyo anakwenda kukata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Wakili huyo alionekana kushindwa kuendelea kusikiliza shauri hilo kwani alinyanyuka alipokuwa amekaa na kutoka nje ya chumba cha mahakama wakati hakimu akiendelea kuwadhaminisha wadhamini.
Washtakiwa hao walitakiwa kuwa na wadhamini wawili kila mdhamini anatakiwa kusaini dhamana ya sh. milioni 30 ambapo walikamilisha masharti hayo.
Kesi itatajwa Novemba 12, mwaka huu na washtakiwa wote wako nje kwa dhamana.
Awali, Mahakama ya Kisutu Septemba 20, mwaka huu iliwafutia mashtaka ya utakatishaji baada ya washtakiwa hao kuonyesha hawana kesi ya kujibu kwenye mashtaka hayo, hivyo wakawa na uwezo wa kupata dhamana.
Baada ya Hakimu Simba kusema hivyo, upande wa mashtaka walidai Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) aliwasilisha hati ya kupinga washtakiwa kupata dhamana.
Viongozi hao wanakabiliwa na mashtaka tofauti yakiwemo ya kughushi pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zachariah Hans Poppe ambaye yeye tangu awali yuko nje kwa dhamana kwani mashtaka yanayomkabili yana dhamana.
Washitakiwa hao awali walikuwa na mashtaka ya utakatishaji mawili pamoja na kughushi ambapo baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi washtakiwa Aveva na Nyange alionekana hawana kesi ya kujibu katika mashtaka ya utakatishaji fedha, bali kwenye makosa mengine ya kughushi nyaraka .
No comments:
Post a Comment