Habari za Punde

SIMBA, EQUITY BANK WAZINDUA KADI YA MASHABIKI 'SIMBA CARD'

Mwenyekiti wa Bodi Benki ya Equity, Raymond Mbilinyi (wa kwanza kushoto), Mkurugenzi Mtendaji, Robert Kiboti na Mkurugenzi wa malipo wa benki hiyo nchini Kenya, Denis Njau, wakisalimiana na baadhi ya wachezaji wa Simba, walipowasili katika Ofisi za Benki hiyo Viwanja vya Julius Nyerere Temeke jijini Dar es Salaam, mwishoni katika hafla ya uzinduzi wa Kadi ya Mashabiki wa Simba 'Simba Card'.  
 Baadhi ya wachezaji wakisajiliwa ili kutengenezewa kadi hizo.
*******************************

Na Muhidin Sufiani
KLABU ya Simba kwa ushirikiano na Benki ya Equity, mwishoni mwa wiki walizindua Kadi mpya ya wanachama wa klabu hiyo itakayowawezesha kuichangia klabu yao na kuitumia kwa matumizi mengine ya Kibenki.
Wanachama wa Simba na mashabiki watanufaika na huduma ya kadi hiyo ikiwa ni pamoja na kuweka, kutoa fedha, kufanya manunuzi ya kieletroniki na kupata punguzo la bei katika maduka na Super Market zitakazoingia ubia na Klabu hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo uliofanyika katika Ofizi za Benki ya Equity zilizopo Viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa bodi wa benki hiyo, Raymond Mbilinyi, alisema kuwa Mabadiliko hayo yataisaidia Simba kuweza kutambua idadi ya mashabiki wake.
Aidha alisema kuwa mashabiki watakaofungua akaunti hiyo wataweza kuitumia Kadi hiyo ya ‘Simba Card’ kwa matumizi ya Kibenki ambayo pia itakuwa haina ulazima wa kubaki na kiwango cha pesa katika akaunti na ambayo haitakuwa na makato ya benki na haina gharama kubwa.
‘’Mashabiki wa Simba wataweza kuitumia kadi hii kwa kufanya manunuzi ya Kieletroniki katika maduka mbalimbali yatakayoingia ubia na Klabnu ya Simba ili kuweza kupata punguzo, kadi hii haitakuwa na makato ya kila mwezi kama ambayo imezoeleka’’. Alisema Raymond
Raymond alisema kuwa miaka miwili iliyopita Klabu ya Simba ilianza kufanya mabadiliko ambayo yameanza kuonekana matunda yake tangu kuanzishwa kwa Klabu hiyo miaka 85 iliyopita ambapo sasa inajisogeza kwa mashabiki kidigitali zaidi.
‘’Benki ya Equity kwa hivi sasa ina jumla ya matawi 15 na mawakala 2500 nchi nzima ambayo yote pia yatakuwa yakitoa huduma kwa mashabiki wa Simba katika kufungua akaunti kupata kadi za mashabiki ili waweze kufaidika na matunda ya Klabu yao pendwa ya kuzidi kujitanua kidigitali’’ alisema Raymond
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingiza Mazingiza, aliwahasa mashabiki kujitokeza kufungua akaunti hiyo ili kuweza kuichangia Simba na baadaye wataweza kuzitumia kadi hizo kununua tiketi za kuingilia Uwanjani. 
Aidha alisema kuwa kuzinduliwa kwa kadi hiyo ni mwanzo wa kuifanya samba ijitegemee kiuchumi ambapo wafanyakazi na wachezaji wote wa Simba wataanza kulipwa mishahara yao kupitia Benki ya Equity.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.