Mkurugenzi wa Kampuni ya SportPesa Tanzania, Abbas Tarimba (kulia) akizungumza wakati wa hafla fupi ya kutiliana saini mkataba wa udhamini na timu Namungo FC kwa kipindi cha mwaka mmoja, katika Ofisi za SportPesa jijini Dar es Salaam, leo. Katikati Mwenyekiti wa Namungo Fc, Hassan Zidadu na Nahodha wa timu hiyo, Reliants Lusajo. (Picha na Muhidin Sufiani).
****************************
Na AMINA KASHEBA
Kampuni ya SportPesa Tanzania, leo imesaini mkataba wa kuidhamini timu ya Namungo Fc kwa mwaka mmoja baada ya kuonesha jitihada katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza Dar es Salaam leo Mkurugenzi Mkuu wa Sportpesa, Abbas Tarimba alisema mkataba huo hauna masharti yoyote kwa timu hiyo zaidi ya kuongeza juhudi katika michunao.
“Tumeingia mkataba wa kuidhamini Namungo Fc kutokana na kuwaona tangu walipopanda ligi Kuu bara na jitihada zao katika kupambana endapo tutapendezwa na klabu hii tutasaini mkataba zaidi ya huu tulioasaini leo'' alisema Tarimba
Aliongezea kuwa Namungo FC wamekuwa wapya katika Ligi Kuu lakini wameonyesha uwezo wa hali ya juu katika kupambania nafasi waliojiwekea katika kikosi chao.
Mwenyekiti wa Namungo FC, Hassan Zidadu alisema timu hiyo imekuwa changa katika Ligi Kuu hivyo wanahitaji kujifunza mambo mbalimbali ambayo yatawawezesha kufanya vizuri msimu ujao.
“Kwasasa hatuhitaji ushindi zaidi ya kubaki katika nafasi za juu katika msimamo wa Ligi Kuu kumi bora ili tuweze kujifunza mambo mbalimbali ambayo yatatuwezesha kupata matokeo mazuri msimu ujao, lakini mkataba huu utasaidia kulipa mishahara ya wachezaji na mambo mbalimbali yanayohusu timu , na endapo tutafanikiwa hata kutwaa Taji la Ligi kuu tutafurahi tu japo haikuwa katika malengo tuliojiwekea''. alisema Zidadu
Naye Nahodha wa timu hiyo, Reliants Lisajo, alisema kikubwa ni ushirikiano wa ufanyaji kazi vizuri ambao utawawezesha kufikia malengo waliojiwekea katika kikosi hicho.
Namungo ambayo kesho inashuka dimbani katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kukipiga na Mabingwa watetezi, Simba SC inayoongoza katika msimamo wa Ligi Kuu Bara huku Namungo wakiwa katika nafasi ya tano wakiwa na Pointi 26.
Mkurugenzi wa Kamopuni ya SportPesa Tanzania, Abbas Tarimba (katikati) akimkabidhi mkataba wa makubaliano ya udhamini Mwenyekiti wa timu ya Namungo FC, Hassan Zidadu, baada ya kusaini mkataba huo wa kuidhamini timu hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja. Hafla fupi ya kusaini mkataba huo ilifanyika Ofisi za SportPesa jijini Dar es Salaam, leo.Kulia ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka nchini TFF, Wilfred Kidau.
No comments:
Post a Comment