Habari za Punde

TCRA YAZINDUA TUZO ZA KUWATAMBUA WATOA HUDUMA ZA MAWASILIANO 2020

 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Mhandisi. James Kilaba, akizungumza wakati akizindua rasmi Tuzo za kwanza wa watoa huduma za Mamlaka hiyo za mwaka 2020. Uzinduzi huo ulifanyika jana katika ukumbi wa Maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. (Picha na Muhidin Sufiani).
 Meza kuu wakisimama kuashiria uzinduzi huo.
************************************
Na Ripota wa Mafoto Blog
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa mara ya kwanza imeandaa tuzo za kuwatambua watoa huduma za mawasiliano nchini zitakazofanyika Mei 17, mwaka huu huku ikisisitiza ni lazima kwa kila mwenye leseni yao kushiriki.
Tuzo hizo zinajumuisha makundi 15 ikiwemo mtoaji  huduma bora za simu wa mwaka, mtoaji huduma bora  za mtandao wa mwaka,  Televisheni bora ya Kitaifa ya mwaka, Televisheni bora ya Wilaya, Televisheni Mtandaoni, Blogger na watoa huduma za usafirishaji mizigo na vifurushi kitaifa na Kimataifa.
Akitangaza tuzo hizo jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa TCRA, Mhandisi James Kilaba alisema lengo la kuandaa tuzo hizo ni kuwatambua watoa huduma wao na kuchochea  utoaji wa huduma  bora za mawasiliano nchini.
Alisema ni lazima kwa kila mtoaji huduma ambaye amepata leseni ya TCRA kushiriki katika tuzo hizo na kwamba kwa kutokufanya hivyo ni kukataa leseni hiyo.
"Utaratibu wa uandaaji wa tuzo hizi ulianza Julai mwaka jana lengo ni kila kada yenye leseni waweze kushiriki ili kujipima nafasi yao katika kutoa huduma," alisema Kilaba.
Pia alisema malengo mengine ya kuandaa tuzo hizo ni kuboresha utoaji wa huduma na kwamba wateja watapata fursa ya kupiga kura kwa mtoa huduma wake ili kuongeza alama katika mchakato huo. KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA

Alieleza kuwa Mei 17 ya kila mwaka ni Siku ya Mawasiliano na Habari duniani na kwamba wamekuwa wakiadhimisha kwa matukio mbalimbali hivyo, waliona umuhimu wa kuweka tuzo hizo ili kutambua michango ya watoa huduma wote Tanzania.
Alisema watoa huduma hizo wamechochea maendeleo ya sekta ya mawasiliano kwani matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) yanategemewa katika kukuza uchumi wa kati na wa viwanda.
Alifafanua kuwa watoa huduma wengi wamewekeza na kuibua ubunifu wa hali ya juu kama vile uwekaji wa matangazo kwenye Blogs hivyo, maendeleo hayo yanapaswa kutambuliwa ili jamii ione mchango wao.
"TCRA imetoa mwongozo unaotoa maelekezo na taarifa muhimu katika kushiriki kwenye tuzo hizo. Lazima mwenye leseni za TCRA kushiriki kwenye tuzo hizi ili mjipime na msipofanya hivyo, maana yake mnakataa leseni yetu," alisisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Tehama na Huduma TCRA, Connie Francis alisema tuzo hizo zinahusisha makundi 15  ambazo ni mtoaji  huduma bora za simu wa mwaka,  mtoaji huduma bora za mtandao,  Televisheni bora ya Kitaifa ya mwaka, Televisheni bora ya Wilaya, redio bora ya kitaifa ya mwaka, redio ya Mkoa, Wilaya na ya Jamii, Televisheni Mtandaoni, Blogger na watoa huduma za usafirishaji mizigo na vifurushi.
Connie alisema wataanza kupokea maombi kwa njia ya mtandao  za kushiriki kwenye tuzo hizo kuanzia leo hadi Machi 15, mwaka huu ambapo watazipitia na kuchagua maombi yaliyowasilishwa.
"Maombi haya yatumwe kwa http://ictawards.tcra.go.tz. baada ya kuyapitia maombi tutafungua dirisha la kupiga kura ambapo wateja wenu watapata nafasi ya kuwapigia kura kwa njia ya mtandao kuanzia Aprili Mosi hadi 30, mwaka huu pamoja na kutuma ujumbe wa maandishi kwenda namba 15072," alisema Francis.
Pia alisema baada ya upigaji kura watachagua washindi ndipo kutoa tuzo hizo.
Alifafanua kuwa kutakuwa na majaji tisa wa ndani na nje ya nchi na tathmini ya kumpata mtoaji huduma bora wa mwaka utazingatia ubunifu, ubora na ufanisi katika huduma.
Nao watoa huduma kwa nyakati tofauti wamepongeza uandaaji wa tuzo hizo kwamba zitachochea ukuaji wa teknolojia nchini.
Umoja wa watoa huduma za simu ulisema maendeleo ya teknolojia yameongeza watu wanaotumia huduma za fedha kwa njia ya simu  ambapo wamefikia milioni 20.
Katibu wa Umoja wa Wamiliki Blogs nchini, Krants Mwantepele aliwataka kwenye blog kuhakikisha wanajidajili TCRA na kupata leseni ili kushiriki kwenye tuzo hizo kwani watapata fursa nyingi.
Pia alisema elimu bado inahitajika kwa wamiliki wa mtandao hiyo kwani wengi hawajajisajili hivyo, kukiuka sheria zilizowekwa.
 Baadhi ya watangazaji wangongwe wakisoma vijitabu vinavyoelezea maudhui ya tuzo hizo.
 Washiriki wakisoma vijitabu vinavyoelezea maudhui ya tuzo hizo.
 Baadhi ya washiriki wakipitia vijitabu vyenye maudhui ya Tuzo hizo.
 Mdau na mwakilishi wa Bloggers, Krants Mwantepele, akiwasilisha ushuhuda.
Mkurugenzi Mtendaji wa Uhuru Media Group, Ernest Sungura (kushoto) akizungumza jambo na Ofisa wa TCRA, Napalite Maginge, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Tuzo za kwanza za watoa huduma za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA, 2020 uliofanyika leo katika ukumbi wa Maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Wadau Mhariri wa michezo ITV, Amri Masare (kulia) na Boy Plus, wakipozi kwa picha baada ya kuhudhuria uzinduzi huo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.