Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe, akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari
(hawapo pichani), alipokutana nao kutoa taarifa ya kuruhusu anga la Tanzania
kutumika kwa ndege za abiria, biashara na mizigo, jijini Dodoma leo.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini, Mhandisi Julius Ndyamukana (kulia), wakimsikiliza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe (hayupo pichani), jijini Dodoma leo wakati alipokutakana na waandishi wa habari kuruhusu anga la Tanzania kutumika kwa ndege za abiria, biashara na mizigo.
********************************************
Serikali ya Tanzania imefuta rasmi zuio
la safari za ndege baada ya taathimini ya mambukizi ya COVID -19 iliyofanywa
nchini kubaini kupungua kwa maambukizi na idadi ya wagonjwa na kurejesha huduma
za usafiri kama ilivyokuwa awali.
Akifuta zuio hilo jijini Dodoma leo Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe ameziagiza Mamlaka
ya Usafiri wa Anga Nchini (TCAA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA),
Kampuni ya Kusimamia na kuendeleza
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KADCO) na Kampuni ya Ndege Nchini
(ATCL) kuanza kutoa huduma bila kikwazo na kuzingatia taratibu za kiafya zilizotolewa
na Shirika la Afya Ulimwenguni na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Nchini.
“Kupitia Tangazo hili natamka kuwa
ndege zote za kibiashara, misaada, kidiplomasia, dharura na ndege maalum
zinaruhusiwa kuruka na kutua katika viwanja vyetu nchini kama ilivyokuwa awali”
Amesema Waziri Mhandisi Kamwelwe.
Waziri Mhandisi Kamwelwe amezitaka
Taasisi hizo kuhakikisha abiria wote wanaoingia nchini wanapimwa joto ili
kuendelea kujikinga na maambukizi yanayoweza kutokea kutokana na muingiliano wa
watu.
Waziri Mhandisi Kamwelwe ameongeza kuwa
kufunguliwa kwa anga hilo kutarejesha fursa za kibiashara hasa katika eneo la
utalii na kuinua pato la Taifa.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ilitoa tamko la kufunga rasmi
ndege za abiria za mashirika ya ndege ya kimataifa kuingia nchini Mei
2020 baada ya kujiridhisha kuwepo na ongezeko la kuenea kwa Virusi vya Korona
Katika hatua nyingine Waziri Mhandisi
Kamwelwe amesema kwa upande wa Usafiri wa Malori kati ya Tanzania na Rwanda
Serikali za nchi hizo zimekubaliana masharti nane ili kuendelea kudhibiti
kuenea kwa virusi kati ya nchi hizo mbili.
Waziri Mhandisi Kamwelwe amesema pamoja
na mambo mengine Serikali hizo zimekubaliana mizigo inayoelekea Rwanda
kushuhushwa katika vituo maalum ikiwemo Rusumo na Kagitumba isipokuwa mzigo wa
mafuta, Magari yanayokwenda Nchini Demokrasia ya Kongo (DRC) kupitia Rwanda
itasindikizwa bure hadi kwenye mpaka wa Rwanda na DRC.
Magari ya mizigo yataruhusiwa kusafiri
kuanzia sa 12.00 asubuhi hadi 12.00 jioni, kuboresha taratibu za upakiajia na
upakuaji wa mizigo katika mipaka, kupunguza vituo vya kusimama.
Waziri Mhandisi Kamwelwe ameongeza kuwa
madereva wote wanaosafirisha mizigo watapimwa mwanzoni mwa safari na kwenye
mipakani baada ya kuwasili.
Aidha, amewataka wadau wote wa
usafirishaji kuhakikisha changamoto zote zinazowakabili ziwasilishwa Wizarani
ili kufanyiwa kazi kabla ya kuathiri biashara katika mipaka yote nchini.
No comments:
Post a Comment