Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa
Azzan Zungu akisoma tamko juu ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani,
mbele ya waandishi wa Habari hii leo Jijini Dodoma. Kwa mwaka huu maadhimisho
hayo yatafanyika kwa kutumia vyombo vya habari bila kuwapo kwa mikusanyiko.
***********************************************
Na Lulu Mussa, Dodoma.
Serikali imesema kuwa mwaka huu maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani Kitaifa yaliyopangwa
kufanyika Mkoani Lindi tarehe 5 Juni 2020 hayatafanyika kutokanana mlipuko wa
Ugonjwa wa Homa ya Mapafu.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu
wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan katika Mkutano wake na Waandishi
wa habari uliofanyika Jijini Dodoma.
“Kama
mnavyofahamu, Nchi yetu na dunia kwa ujumla inakabiliwa na janga la ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya
corona. Ugonjwa huu unaambukizwa kwa njia mbalimbali ikiwemo mikusanyiko ya
watu. Uwepo wa janga hili umesababisha kusitishwa kwa shughuli zinazohusu
mikusanyiko ya watu wengi.” Zungu alisisitiza.
Kwa muktadha huo, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa
maendeleo wamekubaliana kuwa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani
yatafanyika kwa kutumia vyombo vya habari
pamoja na mitandao ya kijamii
kuelimisha na kuhamasisha jamii kutunza mazingira na kuzingatia njia mbalimbali za kujiepusha na
maambukizi ya ugonjwa wa corona.
“Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa
Mazingira ambao ni UNDP, UNEP, WWF, GIZ, Forum CC, Vodacom Foundation, USAID, nchi
wahisani
pamoja na vyombo vya habari tunahamasisha na kuelimisha jamii
kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi kwa kuhifadhi Mazingira hivyo
kutakuwa na mashindano ya
kuandika insha kuhusu mabadiliko ya tabianchi na mikutano ya kitaalamu itakayofanywa
kwa njia ya mitandao kwa kuzingatia njia mbalimbali za kujiepusha na maambukizi
ya ugonjwa wa Corona” Zungu alisema.
Waziri Zungu
ameikumbusha jamii kuwa hifadhi ya mazingira si kazi ya Serikali pekee yake
bali ni jukumu la kila mmoja katika ngazi zote kuanzia ngazi ya kaya na ametoa
wito kwa vyombo vya habari, taasisi zote za Serikali na asasi za kiraia
kusaidia katika kuhifadhi mazingira.
“Watendaji wote
katika ngazi zote hatuna budi kushirikiana katika kutekeleza kwa ukamilifu
Sheria na Kanuni za hifadhi ya mazingira. Kila mmoja ana wajibu na fursa muhimu
katika kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira hapa nchini.
Ningependa kusisitiza kuwa tushirikiane katika kufanya jitihada mbalimbali ili
kupambana na uharibifu wa mazingira kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kukabiliana
na athari za mabadiliko ya tabianchi.” Waziri Zungu alisisitiza.
Amesema kila
mwananchi akiwajibika katika nafasi yake, tutalinda mazingira yetu na jamii kwa
ujumla. Hivyo, shughuli za maadhimisho ya Siku ya Mazingira hapa nchini mwaka huu
pamoja na mambo mengine, zitalenga kuhamasisha jamii kuhifadhi mazingira na
kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuelimishana jinsi ya kuepuka
maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19.
Kila tarehe 5 Juni, nchi yetu huungana na mataifa
mengine duniani kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani. Maadhimisho
ya Siku ya Mazingira Duniani kitaifa yalipangwa kufanyika mkoani Lindi na Kauli
mbiu ya maadhimisho haya kitaifa ni Tuhifadhi
Mazingira: Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi.
No comments:
Post a Comment