Habari za Punde

OFISI YA WAKILI MKUU WA SERIKALI YAANZA UJENZI WA OFISI KATIKA MJI WA SERIKALI MTUMBA, DODOMA

Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende akikata utepe kwa ajili ya makabidhiano ya nyaraka za ujenzi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inayotarajiwa kujengwa katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma. Wa kwanza kulia ni Mhasibu Mkuu wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, CPA. Devotha Ngulugulu.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende (wa tano kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na wawakilishi wa  Kampuni ya Ujenzi ya SUMA JKT na TBA na watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakati wa makabidhiano ya eneo kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma.
*************************
Na Prisca Ulomi, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Dodoma
Wawakilishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) wakiongozwa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende leo tarehe 18 Juni, 2022 wameshuhudia makabidhiano ya eneo la ujenzi wa Ofisi za Makao Makuu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali lenye  ukubwa wa mita za mraba 17,342. Makabidhiano hayo yamefanyika kwenye Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma baina ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambaye ni Mshauri Elekezi aliyewakilishwa na Msanifu Majengo Weja Ng’olo na Kampuni ya Ujenzi ya SUMA JKT ambae ni Mkandarasi iliyowakilishwa na Mkadiriaji Majenzi, Jacob Ghati.
Akikabidhi eneo hilo, Mwakilishi wa TBA, Ng’olo ameeleza kuwa jengo la Ofisi linalotarajiwa kujengwa ni la kisasa na ni miongoni mwa majengo yenye muonekano mzuri katika Mji wa Serikali Mtumba. Jengo hili litakuwa na miundombinu mbalimbali ikiwemo vyumba vya Ofisi 127, maegesho ya magari 111, maktaba, kumbi 2 za mikutano zenye nafasi 108 kila mmoja, kumbi 2 za kutolea mafunzo zenye nafasi 42 kila mmoja, maabara ya kompyuta, vyumba vidogo 10 vya mikutano na chumba cha akina mama wanyonyeshao. Ujenzi wa jengo hilo unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi kumi na nane (18). 
Akizungumza kwa niaba ya Mkandarasi, Gati amesema kuwa wako tayari kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa mujibu wa mkataba na kwa kushirikiana na Mshauri Elekezi (TBA) na Mshitiri (OWMS).
Kwa upande wake, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Luhende amewatakia Mkandarasi na Mshauri Elekezi utekelezaji mwema wa majukumu yao kwa mujibu wa mkataba na kwa kuzingatia weledi. Pia amewahakikishia kuwa Ofisi ya Wakili Mkuu Serikali itawapa ushirikiano unaostahili.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende (aliyesimama katikati) akiwa na wawakilishi wa Kampuni ya Ujenzi ya SUMA JKT na TBA pamoja na baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali baada ya hafla fupi ya kukabidhi eneo la ujenzi wa jengo la makao makuu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali lililopo Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende (wa tatu kulia) akipata maelezo kutoka kwa mwakilishi wa TBA, Msanifu Majengo Weja Ng’olo na Mwakilishi wa SUMA JKT, Jacob Gati (wa kwanza kushoto) wakati wa makabidhiano ya eneo la ujenzi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwenye Mji wa Serikali Mtumba Dodoma.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende (wa pili kulia) akishuhudia wawakilishi wa TBA wakiwaonesha mipaka wawakilishi wa Kampuni ya Ujenzi  ya SUMA JKT. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Bw. James Kibamba na kulia ni Mkurugenzi wa Mipango, Dkt. Abdul Mussa.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.