Habari za Punde

WAZIRI MHAGAMA ATAKA VIPAJI VYA SHIMIWI VIENDELEZWE

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala bora, Mhe.Jenista Mhagama akizungumza na baadhi ya wanamichezo wa Sekta ya Uchukuzii, mara baada ya  Ufunguzi wa Mashindano ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), jijini Tanga.
Wanamichezo kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Wakipita mbele ya Mgeni Rasmi  Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala bora, Mhe. Jenista Mhagama, wakati wa ufunguzi wa mashindano ya Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), Jijini Tanga.  
Wachezaji wa Timu ya Kuvuta Kamba Kutoka Sekta ya Uchukuzi, (wenye sare ya bluu) wameibuka kidedea mara baada ya kuwafunga timu ya Hazina kwa kuwavuta raundi zote mbili, mchezo ulioshuhudiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala bora, Mhe. Jenista Mhagama, wakati wa ufunguzi wa Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), Jijini Tanga.

Na Mwandishi Wetu, Tanga

WAZIRI wa Ofisi ya Rais ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama amevitaka vipaji vya wachezaji wa michezo mbalimbali kwenye michezo ya Sjhirkisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali, (SHIMIWI), viendelezwe na kutumika kwenye timu za taifa nchini.

Mhe. Mhagama ametoa kauli hiyo katika ufunguzi rasmi wa michezo ya SHIMIWI inayofanyika Jijini Tanga akimwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, ambapo  amesema watumishi wa umma wanaoshiriki kwenye michezo hii wameonesha vipaji vya juu ambavyo vitaweza kusaidia taifa na timu mbalimbali za hapa nchini. SHIMIWI inashirikisha michezo ya soka, netiboli, kuvuta kamba, mbio za baiskeli, raidha, karata, bao, draft na vishale (darts).

“Hakuna sababu ya kwenda nje ya nchi kutafuta wachezaji kwani hata kina Mayele na Leta Mzungu unaweza kuwakuta ndani ya Ofisi ya Rais Ikulu na Madini, na wamo wengi sana humu humu kwenye timu zetu zinazoshiriki SHIMIWI, hivyo vipaji vyao viendelezwe zaidi,” amesema Mhe. Mhagama

Amesema SHIMIWI inaendelea kukua kwa kushirikisha timu nyingi kutoka kwenye wizara, Idara, Wakala za serikali na Ofisi za Wakuu wa mikoa na atahakikisha anapeleka salamu serikalini ili mikoa yote ishiriki kwenye michezo hii, tofauti na mwaka huu imeshiriki mikoa 18 pekee.

Halikadhalika Mhe. Mhagama amesema baada ya timu za SHIMIWI kuendelea kuwa bora na wabobezi zitaweza kushindana na timu za serikali za nchi nyingine kwenye  michezo makubwa ya umoja wa Afrika Mashariki, ili kujenga urafiki.   

Pia amelitaka shirikisho hilo  kuhakikisha watumishi wenye mahitaji maalumu wanashiriki kikamilifu kwenye michezo ijayo.

"Napenda kuwahamasisha Watumishi wa Umma wenye mahitaji maalum kushiriki michezo hii, mwakani na idadi ya Watumishi iongezeke zaidi na kuongeza baadhi ya michezo ambayo haipo kwa sasa kama kabadi ili washiriki kikamilifu haki hii ya msingi," amesema Mhe. Mhagama.

Mhe. Mhagama amewagiza waajiri wote nchini kuhakikisha wanamichezo wanawezeshwa vyema kushiriki michezo hiyo, huku akitaka wanamichezo kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za michezo pamoja na Utumishi wa Umma.

Katika Hatua nyingine Mhe.Mhagama amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha maslahi ya Watumishi wa Umma, ikiwemo upandaji wa madaraja, ubadilishaji wa kada na kufuta tozo ya thamani ya Mkopo wa Elimu ya Juu.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa SHIMIWI, Daniel Mwalusamba amesema shirikisho linakabiliwa na changamoto la kukosa utaratibu wa kushiriki kwenye mazoezi, ambapo ameomba uwekwe utaratibu ili waweze kushiriki kwa wingi.

Amesema malengo ya SHIMIWI ni kujenga umoja wa kitaifa, kujenga ushindani wa kimichezo kati ya watumishi na taasisi zake, kujenga afya ya kimwili na akili na kujenga ukakamavu na moyo wa ushindani na kuwafanya watumishi kuwa na mahusiano mazuri na kufahamiana.

Mwalusamba amesema michezo ya mwaka huu imeshirikisha wanamichezo 2510 wanashiriki kwenye michezo hiyo, kutoka kwenye timu timu 63 kutoka Wizara 27, Mikoa 18, Idara za Serikali 18 zinashiriki michezo hiyo iliyobeba Kauli mbiu  "Michezo hupunguza magonjwa yasiyoambukiza na kuongeza tija  mahala pa kazi, Kazi Iendelee".

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.