Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa (wa tatu kulia) akimkabidhi Tuzo ya mshindi wa kwanza wa Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika, Dotto Daudi, wakati wa hafla ya utoaji tuzo hizo iliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam, leo. (kulia) ni Mkuu wa MKoa wa Dar es Salaam, Amosi Makala (wa pili kulia) ni Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mohammed Mchengerwa. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa AlAF Tanzania, Ashish Mistry na Mkurugenzi Mtendaji wa Safal Group, Andrew Lindgren. (Picha na Muhidin Sufiani)
...........................................................
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa maagizo sita yanayolenga kukuza na kueneza lugha ya kiswahili, kiwemo kuitaka Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuhakikisha unakuja na mpango mkakati utakasaidia kueneza na kukuza matumizi ya lugha hiyo ndani na nje ya nchi.Pia, ameiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kushirikiana na Wizara ya Utamaduni kuhakikisha bidhaa zote zinazozalishwa nchini na zinazoingizwa kutoka nje ya nchi zinakuwa na maelezo ya matumizi yake kwa lugha ya Kiswahili.
Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo Dar es Salaam jana katika hafla ya kutoa Tuzo ya Kiswahili ya Safal-corneal ya Fasihi ya Afrika iliyoandaliwa na Kampuni ya Mabati ya Alaf Tanzania.
Alitaja maagizo mengine kuwa ni kuitaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikiana na wadau kuhakikisha lugha ya Kiswahili inakua na kueneo duniani kote pamoja na Tanzania kuendelea kuwa kinara wa lugha hiyo.
Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa aliagiza Wizara ya Utamaduni kuanzisha Tuzo maalumu ya Kazi za Kiswahili katika Sayansi na Teknolojia kama ilivyopendekezwa na wadau kupitia jukwaa hilo la tuzo za Safal-Cornel za Fasihi ya Afrika.
“Kwa upande wa Wizara ya Viwanda hakikisheni kwamba bidhaa zote zinazozalishwa katika viwanda vya hapa nyumbani na zile zinazoingizwa nchini kutoka nje zinakuwa na maelezo yaliyotolewa kwa lugha ya Kiswahili. Kufanya hivyo, kutawafanya watumiaji wa bidhaa hizo wazitumie wakiwa wanafahamu vyema maelekezo yaliyomo kwenye bidhaa hizo,” alisema.
Alizitaka pia, Mamlaka husika zisimamie kuhakikisha Lugha ya Kiswahili inatumika katika maeneo mbalimbali ikiwemo; maelekezo ya dawa hospitali, matangazo, alama za barabarani na majina ya shule na hoteli.
Aidha, aliagiza mamlaka husika kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na viongozi waandamizi kwa nyakati tofauti kuhusu kueneza lugha hiyo na kuanzisha mpango mkakati wa utekelezaji wake.
“Kwa mfano, Julai 7, 2022 wakati wa maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Kiswahili Duniani Mheshimiwa Dk Philip Mpango, Makamu wa Rais alitoa maagizo ambayo yanahitaji hatua za utekelezaji. Hakikisheni mnatekeleza ipasavyo maagizo hayo kwani iwapo yatatekelezwa kikamilifu, ninaamini lugha ya Kiswahili itakuwa imepiga hatua kubwa sana,” alisisitiza.
Alitoa wito kwa asasi zinazohusika na maelekezo aliyoyatoa Dk Mpango pamoja na maelekezo aliyoyatoa jana kufanya tathmini ya utekelezaji ili kuyaripoti katika maadhimisho yajayo ya Siku ya Kiswahili.
Aidha, aliagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikiana na na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuandaa mitaala mipya ya elimu itakayosaidia kukuza kiswahili kwa kuyashirikisha makundi mbalimbali ikiwemo wanawake na vijana.
Awali, Waziri Mkuu huyo alitoa msisitizo wa mambo matatu ya kuzingatiwa katika ukuzaji na uenezaji wa Kiswahili na kuagiza kuwe na mkakati wa kutangaza Kiswahili ndani na nje ya nchi kwa kuandika na kusambaza kamusi na vitabu vya Kiswahili vitakavyowasaidia watu kujifunza lugha hiyo adhimu.
" Wataalamu wa Kiswahili hakikisheni mnaweka mikakati thabiti ya kupenyeza Kiswahili nje ya nchi kwa njia mbalimbali… Vilevile, sambazeni vijitabu vyenye misamiati muhimu kwa wasomaji wa awali wa lugha ya Kiswahili, viwekeni kwenye mitandao ili viweze kusomwa na watu wengi zaidi duniani,” alieleza.
Alihimiza Kiswahili kutumika katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja huduma za jamii, mikutano, warsha na makongamano; na kuagiza tafiti za lugha ya Kiswahili kuimarishwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohammed Mchengerewa alisema Kiswahili ndio lugha kuu nchini inayowaunganisha watanzania wenye makabila zaidi ya 150.
Alisema kwa sasa lugha hiyo inaenea kwa kasi duniani na ni moja klati ya lugha 10 mashuhuri duniani. “Lakini bado kasi ya usambazaji wake haijakua ikiwemo fursa nyingi za lugha hiyo nje ya mipaka ya Tanzania ambazo bado hazijatumiwa vizuri. Tuna kazi kubwa ya kuyafanikisha haya,”
Mkurugenzi Mkuu wa Alaf Tanzania Ashish Mistry alisema kampuni hiyo imekuwa ikidhamini tuzo hizo kwa muda mrefu tangu zianzishwe mwaka 2015 na sasa imeongeza udhamini hadi kwa wanafunzi wa shahada ya umahiri ya Kkiswahili kupitia chuo kikuu cha Dar es salaam takribani 12.
Washindi wa tuzo hizo waliobuka kinara wote ni Watanzania. Mshindi wa kwanza kwa upande wa riwaya ni Doto Rangimoto na mshindi wa kwanza katika ushairi ni Salum Makamba ambao wote wamejinyakulia dola za Marekani 5,000 sawa na Sh milioni 11.6.
Mshindi wa pili katika riwaya ni Isaac Ndolo na wa pili katika ushairi ni Ally Mchanyato ambao wote wamejinyakulia dola za Marekani 2,500 sawa na Sh milioni 5.8.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa (wa tatu kulia) akimkabidhi Tuzo ya mshindi wa kwanza wa kwa upande wa Ushahiri Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika, Salum Makamba, wakati wa hafla ya utoaji tuzo hizo iliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam, jana. (kulia) ni Mkuu wa MKoa wa Dar es Salaam, Amosi Makala (wa pili kulia) ni Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mohammed Mchengerwa. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa AlAF Tanzania, Ashish Mistry na Mkurugenzi Mtendaji wa Safal Group, Andrew Lindgren.
Mpiga Kinanda wa Bendi ya Muziki ya Bahati Fimale, Nipael Mtana, akipiga Kinanda kwa umahiri wakati bendi yake ilipokuwa ikitoa burudani kwenye hafla ya utoaji Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City Dar es SalaamMsanii wa Kikundi cha Sanaa cha Wanne Star, Hassan Michael, akionyesha umahiri wake wa kujinyonganyonga kama hana mifupa, jukwaani mbele ya mgeni rasmi Waziri Mkuu (hayupo pichani) wakati wa hafla ya utoaji tuzo Tuzo za Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika iliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam,Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, akimkabidhi zawadi ya pesa taslimu Tsh. 100,000 msanii wa Kikundi cha Sanaa cha Wanne Star, Hassan Michael kwa kumpongeza baada ya kuonyesha sanaa yake jukwaani na kukonga nyoyo za mashabiki waliokuwapo ukumbini hapo kwa kujinyonganyonga kama hana mifupa.
No comments:
Post a Comment