Habari za Punde

NMB YAKABIDHI VITANDA, MAGODORO NA WHEEL CHAIR KWA ZAHANATI YA UNUNIO

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Charles Lawisso (wa tatu kulia) akipokea msaada wa Vitanda vya wagonjwa kutoka kwa Meneja Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam, Ferdinand Mpona, wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa hivyo kwa ajili ya Zahanati ya Ununio, iliyofanyika katika Zahanati hiyo jijini Dar es Salaam , jana. Kulia ni Diwani wa Kata ya Kunduchi, Michael Urio (wa pili kulia) ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ununio, Mwinjuma Mwinyi.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Charles Lawisso (wa tatu kulia) akipokea msaada wa Vitanda vya wagonjwa kutoka kwa Meneja Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam, Ferdinand Mpona, wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa hivyo kwa ajili ya Zahanati ya Ununio, iliyofanyika katika Zahanati hiyo jijini Dar es Salaam , jana. Kulia ni Mganga Mfawidhi wa Zahanati hiyo, Happyness Mbeyela (wa pili kulia) ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ununio, Mwinjuma Mwinyi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ununio, Mwinjuma Mwinyi, (wa pili kulia) akipongezana na Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Ununio, Happyness Mbeyela, baada ya kukabidhiwa msaaada wa vitanda vya wagonjwa vya Zahanati ya Ununio iliyopo Kata ya Kunduchi jijini Dar es Salaam, jana. Katikati yao ni Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam, Ferdinand Mpona na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Charles Lawisso (wa pili kulia) wakishuhudia
Meneja Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam, Ferdinand Mpona, akizungumza wakati wa hafla hiyo
Diwani wa Kata ya Kunduchi, Michael Urio, akizungumza wakati wa hafla hiyo

Na Julieth Innocent na Sauda Michael DSJ

KUPITIA Programu ya Uwekezaji kwa Jamii (CSI), Benki ya NMB imekabidhi msaada wa vitanda vitano na magodoro yake, vikiwamo vinne vya kulala wagonjwa, kimoja cha kufanyia uchunguzi wa awali, pamoja na kiti cha magurudumu ‘wheel chair’ cha kubebea wagonjwa kwa Zahanati ya Ununio.

 

Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika Jumatatu Mei 27, katika Zahanati ya Ununio, Kata ya Kunduchi, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, ambako Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Ferdinand Mpona, alimkabidhi Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Charles Lawisso.

 

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mpona alisema afya na elimu ni kati ya Sekta za Kipaumbele kwa NMB, ambazo zimekuwa zikitumia kiasi kikubwa cha asilimia moja ya faida baada ya kodi ya benki hiyo kwa kila mwaka, inayotengwa kusaidia utatuzi wa changamoto kwenye nyanja hizo.

 

“Changamoto za Afya na Elimu kwa benki yetu ni jambo la kipaumbele na hii ni kutokana na ukweli kwamba nyanja hizo ndio msingi wa maendeleo ya taifa lolote, ndio maana sisi hutenga asilimia moja ya faida yetu kila mwaka kusaidia sekta hizo pamoja na majanga.

 

“Tunatambua juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kusimamia upatikanaji wa elimu na afya bora mijini na vijijini, ambako imejikita katika kuboresha utoaji huduma hizo, nasi tukiwa wadau muhimu, tunao wajibu wa kuunga mkono,” alisema Mpona.

 

Alibainisha ya kwamba, kwa miaka kadhaa NMB imekuwa ikisaidia miradi ya maendeleo kwa jamii ikijielekeza zaidi katika elimu – inakotoa misaada ya madawati, vifaa vya kuezekea na ujenzi, pamoja na afya inakochangia vifaa tiba vikiwemo vitanda, magodoro, mashuka na mashine za uchunguzi.

 

“Tunafanya hivi tukitambua kwamba kupitia jamii ndipo wateja wetu wote hutoka na hivyo ni sahihi kwetu na ni utamaduni endelevu kurejesha kwa jamii kupitia CSI (ambayo zamani ilikuwa ikitambulika kama CSR),” alisema Mpona mbele ya wafanyakazi wa zahanati hiyo kongwe.

 

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Charles Lawisso, aliishukuru NMB kwa juhudi za wazi katika maeneo mbalimbali nchini, ambako imejitoa kusapoti juhudi za Serikali katika kutatua changamoto zinazokwaza ustawi wa sekta hizo za kimkakati.

 

“Serikali imefanya na inaendelea kufanya makubwa katika afya, lakini hiyo haiondoi ukweli kuwa inahitaji sana uungwaji mkono na ndio maana tunaishukuru sana NMB kwa sababu imechagua kusapoti jitihada hizo kwa vitendo kupitia asilimia moja ya faida yao kwa mwaka.

 

“Tunawashukuru tena na tena kwa msaada huu mnaokabidhi hapa leo na mingine mingi mliyotoa kila kona ya nchi hii, ambako wote tunashuhudia kila uchao mkifanya jitihada kubwa kutatua changamoto hizi. Tunawaomba muendelee na moyo huu.

 

“Risala imetaja changamoto nyingi zilizopo katika zahanati hii, bado tunawahitaji tukiamini vifaa hivi mnavyotoa vinachochea ufanisi miongoni mwa wafanyakazi wa zahanati zetu na kuboresha afya za wananchi wetu,” alisema Lawisso mbele ya Diwani wa Kunduchi, Michael Urio.

 

Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Ununio, Dk. Happiness Mbeyela, alisema zahanati hiyo iliyojengwa kwa awamu mbili – ya kwanza ikijengwa mwaka 1986 na ya pili mwaka 1997, inahudumia zaidi ya wananchi 37,302.

 

“Hiyo ni idadi ya wakazi wa maeneo ya Ununio, Kwa Kondo, Pwani na mitaa ya jirani ikiwemo ya Boko, Mbweni, Tegeta na Kunduchi. Zahanati hii yenye watumishi 10, ina changamoto mbalimbali zikiwemo za uzio, uchakavu wa majengo na ukosefu wa mashine ya ‘ultra sound.’

  

“Tunapenda kuishukuru NMB kwa msaada huu wa vitanda vya kulala wagonjwa na kiti cha magurudumu, ambao umekuja kwa wakati sahihi, hasa baada ya kukamilika kwa jengo la wazazi, ambalo linaenda kusaidia maboresho ya afya ya mama na mtoto,” alisema Dk. Mbeyela.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.