KUPITIA Programu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), Benki ya NMB wiki iliyopita imekabidhi msaada wa vifaatiba vyenye thamani ya Sh. Mil. 16 kwa Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo mkoni Pwani na Zahanati ya Ununio, iliyopo wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam
Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Ferdinand Mpona, ndiye aliyekabidhi viti vya magurudumu ‘wheel chair’ 21, vitanda 10 vikiwamo vya kujifungulia vitano na vya kulala wagonjwa vitano kwa Wakurugenzi wa Wilaya hizo Shauri Selenda na Charles Lawisso, kwa niaba ya wakuu wa wilaya zao.
Mjini Bagamoyo, Mpona alikabidhi ‘wheel chair’ 20 na vitanda vitano vya kujifungulia vyenye thamani ya Sh. Mil. 10 kwa Mkurugenzi Selenda, huku Lawisso akipokea vitanda vinne vya kulala wagonjwa, kimoja cha kufanyia uchunguzi wa awali na ‘wheel chair’ moja vyenye thamani ya Sh. Mil. 6.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Halima Habibu, Mkurugenzi Selenda aliishukuru NMB kwa kuyapa thamani majengo yaliokarabatiwa na Serikali kwa gharama ya Sh. Milioni 900 kwa kukabidhi viti 20 vya kubebea wagonjwa na vitanda vitano vya wazazi.
“Tunawashukuru na kuwapongeza NMB kwa hiki mnachokifanya katika Sekta ya Afya, Serikali inafanya makubwa mno, kwa mfano hapa imetuletea Sh. Milioni 900 za ukarabati wa majengo haya, nanyi mkaona msapoti juhudi hizo kwa kuleta vifaatiba hivi.
“Licha ya kutumia gharama kubwa kama hiyo, lakini ukarabati huu waweza kuwa si lolote, si chochote iwapo ndani ya majengo haya wagonjwa watalala chini, watakosa huduma sahihi na rafiki, ndio maana tunahitaji sana nguvu za wadau muhimu kama nyie,” alisema Selenda katika hafla hiyo.
Kwa upande wake, Mpona alisema msukumo wa taasisi yake kusaidia vifaa hivyo ni kutokana na ukweli kwamba Sekta ya Afya ni moja ya vipaumbele vya benki yake na kwamba wanatambua na kuthamini jitihada za Serikali katika Nyanja hizo, ndio maana wanajisikia Fahari kuunga mkono.
“Afya kama ilivyo Elimu ni Sekta za Kipaumbele kwa NMB, tunatambua na kuthamini jitihada za Rais wa Awamu ya Sita, Dk. Samia Suluhu Hassan, ndio maana sisi tunafurahi tunapokimbiliwa kuombwa misaada hii ambayo tunaitengea asilimia moja ya faida yetu kila mwaka.
“Kimbilio lenu kwetu sisi linaakisi imani yenu kwetu. Linathibitisha mnavyothamini mchango wetu na mnavyotuamini, nasi tunajivunia sana jambo hilo.
"Na leo tuko hapa kukabidhi viti vya magurudumu vipatavyo 20 kwa ajili ya kupokelea, kutembezea wagonjwa waanapotoka sehemu moja kwenda nyingine na vitanda vya kujifungulia vitano vyenye thamani ya Sh. Mil. 10,” alibainisha Mpona.
Hafla ya makabidhiano hayo ilihudhuriwa na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Dk. Kandi John Lussingu, aliyeshuhudia Mkurugenzi Selenda akiipokea, kisha naye kukabidhi vifaatiba hivyo kwa Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, Dk. Rehema Lukwaro
Katika hafla ya mapema kwenye Zahanati ya Ununio, iliyopo Kata ya Kunduchi, wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Lawisso, aliishukuru NMB kwa juhudi za wazi katika maeneo mbalimbali nchini, ambako imejitoa kusapoti juhudi za Serikali kutatua changamoto za afya.
“Serikali imefanya na inaendelea kufanya makubwa katika afya, lakini hiyo haiondoi ukweli kuwa inahitaji sana uungwaji mkono na ndio maana tunaishukuru sana NMB kwa sababu imechagua kusapoti jitihada hizo kwa vitendo kupitia asilimia moja ya faida yao kwa mwaka.
“Risala imetaja changamoto nyingi zilizopo katika zahanati hii, bado tunawahitaji tukiamini vifaa hivi mnavyotoa vitachochea ufanisi miongoni mwa wafanyakazi wa zahanati yetu na kuboresha afya za wananchi wetu,” alisema Lawisso mbele ya Diwani wa Kunduchi, Michael Urio.
No comments:
Post a Comment