Habari za Punde

MHE. MARTINE SHIGHELLA AHIMIZA JAMII KUJENGA UTAMADUNI ENDELEVU WA KUPANDA MITI

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja akipanda mti katika eneo la Hospitali ya Rufaa ya Kanda- Chato Mkoani Geita ikiwa ni maadhimisho ya siku ya usafi wa mazingira nchini.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja (kulia) akiwa pamoja na Katibu Tawala Wilaya ya chato Mkoani Geita, Bw. Thomas Dimme (kushoto) wakifanya usafi wa mazingira katika eneo la Hospitali ya Rufaa ya Kanda- Chato ikiwa ni maadhimisho ya kitaifa ya usafi wa mazingira nchini 
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja (kulia) akiongozana na Katibu Tawala Mkoa wa Geita Bw. Mohamed Gombati kufanya usafi wa mazingira katika eneo la Hospitali ya Rufaa ya Kanda- Chato Mkoani Geita ikiwa ni maadhimisho ya siku ya usafi wa mazingira kitaifa
Mkuu wa mkoa wa geita, mhe. Martine Shighella akipanda mti katika eneo la Hospitali ya Rufaa Kanda ya Chato wakati wa maadhimisho ya siku ya kitaifa ya usafi wa mazingira tarehe 1 juni, 2024. Wanaoshuhudia ni Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mhe. Said Mkumba na Mbunge wa Chato, Mhe. Medard Kalemani
MKUU wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigella amehimiza jamii kujenga utamaduni endelevu wa kupanda miti kwani kwa sasa ni fursa ya kibiashara inayolenga kukuza kipato cha kaya, familia na taifa kwa ujumla.
Mhe. Shigella ametoa rai hiyo tarehe 1 Juni, 2024 Wilayani Chato Mkoani humo wakati wa zoezi la usafi wa mazingira lililofanyika katika eneo la Hospitali ya Rufaa ya Kanda- Chato ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Mazingira Duniani itayofanyika tarehe 5 juni mwaka huu.
Mhe. Shigella amesema uhifadhi wa mazingira inaenda sambamba na zoezi la upandaji miti ambapo kwa sasa kumebua fursa ya biashara ya kaboni na hivyo kuhimiza jamii kupanda miti kwa wingi katika maeneo yao ili kuweza kujiongeza kipato. 
Ameeleza kwa sasa mti ni fursa ya kibiashara kwani ukipandwa na kustawi unaongeza kipato kupitia kaboni na kuwataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo ambayo pia itatimiza dhamira ya kupanda miti milioni 1.5 kwa mwaka katika kila halmashauri inafikiwa na kuhimiza wajibu kwa viongozi na watendaji wa Serikali kusimamia utekelezaji wa maagizo hayo.
Kwa mujibu wa Shighella ameeleza kuwa suala la upandaji miti kwa sasa limepewa msukumo na kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Sita ambapo kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imeandaa kanuni na miongozo ya usimamizi wa biashara ya kaboni inayolenga kuwanufaisha wananchi.
Amefafanua kuwa ili kufikia malengo ya upandaji miti ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha anajenga utamaduni wa kupanda miti katika maeneo ya makazi, ikiwemo nyumba za ibada, maeneo ya masoko, vituo vya afya n.k.
Aidha Shighella ameeleza kuwa kutokana na fursa zilizopo kupitia kaboni, Mkoa huo upo mbioni kuandaa mkutano wa wadau wa mazingira ikiwahusisha viongozi wa serikali na wawakilishi wa wananchi ili kujadiliana mbinu na mikakati inayolenga kuwanufaisha wananchi. 
Pia Mhe. Shighella amewasihi wananchi kuachana na shughuli zisizo endelevu ikiwemo uchimbaji holela wa madini ambao umekuwa ukisababisha athari kwa mazingira ikiwemo ukataji miti na kuwahimiza wasimamizi wa maeneo ya migodi kuhakikisha wanapanda miti ili kurejesha na kutunza uoto wa asili.
“Tuna wajibu wa kurejesha na kutunza uoto wa asili uliopo nchini kwani utunzaji wa  mazingira ni jambo muhimu linalobeba mustakabali wa maisha ya vizazi vya sasa na vijavyo sambamba na kutunza mifumo ekolojia iliyopo majini na ardhini” amesema Shigella.       
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja ameupongeza Mkoa wa Geita kwa juhudi mbalimbali inazoendelea kuzifanya katika kusimamia masuala ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira ikiwemo usafi na upandaji miti.
Ameongeza kuwa uwepo wa changamoto ya mabadiliko ya tabianchi umeibua fursa ya kipato na kiuchumi kwa jamii kupitia kaboni inayotokana na faida ya upandaji miti, ambapo kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa kuandaa kanuni na miongozo ya usimamizi wa biashara hiyo.
Mhandisi Luhemeja amesema ili kuhakikisha jamii inanufaika na fursa zilizopo katika kaboni, Serikali imeendelea kutoa elimu kwa viongozi wa serikali za mitaa, wabunge na makundi mbalimbali wakiwemo wawekezaji.  
“Miti kwa sasa ni biashara hivyo kutokana na umuhimu uliopo, Serikali inahamasisha biashara ya kaboni……Kuelekea Siku ya Mazingira Duniani Juni 5 mwaka huu tutatoa hundi ya shilingi Bilioni 14 kwa halmashauri ya Tanganyika, Mkoani Katavi ambayo inafanya biashara hii” amesema Mhandisi Luhemeja.   
Nae Mbunge wa Chato, Mhe. Medard Kalemani ameishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuichagua Wilaya hiyo kuongoza shughuli za usafi wa mazingira katika Mkoa wa Geita na kueleza viongozi na watendaji wamejipanga vyema kutekeleza kwa vitendo dhamira ya Serikali ya kupanda miti na kusimamia usafi wa mazingira.
“Wilaya ya Chato tumejiwekea mkakati kwa kuhakikisha tunapanda miti isiyopungua 1000 kwa mwaka ili kutunza mazingira na tayari tuna msitu wa Silayo ambapo hadi sasa tumepanda miti ekari 98,000 na miti yote ipo katika hali nzuri na inaendelea kutunzwa” amesema Mhe. Kalemani.  
Tarehe 5 Juni ya kila mwaka Tanzania huungana na Jumuiya ya Kimataifa katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani. Kauli Mbiu ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka 2024 inasema “Urejeshwaji wa Ardhi, Ustahimilivu wa Hali ya Jangwa na Ukame”

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.