Habari za Punde

MNYAMA KUONDOLEWA ‘BIKIRA’ KESHO?

Mrisho Ngasa akimtesa beki wa Simba Kelvin Yondan.
Na SPM

TIMU ya Simba ya jijini Dar es Salaam, kesho itashuka dimbani kuwakabili watani wake wa Jadi Yanga, huku ikiwa na rekodi nzuri ya kutofungwa na timu yeyote katika michezo yake iliyokwishacheza katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara huku ikiwa kileleni katika ligi hiyo kwa kuwa na pointi 27 wakifuatiwa na Mahasimu wao wanye Pointi 18 sawa na Mtibwa wanaotofautiana magoli ya kufungwa.

Maswali mengi yaliyotawala miongoni mwa mashabiki wa soka hii leo ni je Mnyama huyo yupo tayari kutunza ‘ujana wake na kuuachia kirahisi kwa aliyejitokeza kutoa posa kwa ajili yake na kupata pointi tatu muhimu kutoka mikononi mwake’.

Hii imefananishwa na Binti anayeweza kujitunza katika usichana wake lakini akiamini kuwa ipo siku atampata mwenza aliyemuamini na kuamua kumtunuku na kumkabidhi funguo za kufungua kufuli la nyumba ya maisha yake.

Lakini pia inawezekana mwanaume anayejitokeza kutoa posa akawa hajakamilisha vigezo vinavyoweza kuwashawishi wazazi ili kukabidhiwa binti na matokeo yake binti huyo akaendelea kubaki na kusubiri atakayejitokeza na kutimiza vigezo vyote ili kuachiwa point tatu.

Haya yote yanaweza kutokea leo ikiwa ni pamoja na majigambo ya hapa na pale ya mashabiki na viongozi wa timu za Watani wa Jadi Yanga na Simba zote za jijini Dar es Salaam, lakini bado muamuzi wa tambo zote atabakia kuwa ni dakika 90 za mchezo kati ya mahasimu hao wawili utakaochezwa leo kwenye Uwanja Mkuu wa Taifa jijini.

Kumekuwa na tambo kadhaa huku kila mmoja akitamba kumfunga mwenzake, na leo ni miezi 12, tangu timu hizo zilipokutana katika mzunguko wa kwanza wa ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara, ambapo Yanga ilishinda bao 1-0, goli hilo likifungwa na Ben Mwalala, na pia ni miezi 7 sasa toka timu hizo zikutane katika mzunguko wa pili wa lgili hiyo huku mahasimu hao wakitoshana nguvu kwa kufungana 2-2.

Leo kila timu itaingia uwanjani huku kila moja ikijitahidi kufanya iwezavyo ili kuepuka fedheha ya kufungwa ya kwanza na mwenzake kwa msimu huu, ili kuweka rekodi nzuru katika na kujiweka katika nafasi nzuri kabla ya kukutana katika mzunguko wa pili.

Ikiwa ni pamoja na maandalizi ya kutosha na ya vitisho yaliyokuwa yakifanywa na timu zote huku kila moja ikijitahidi kufanya lile ambalo inadhani itakuwa ni tishio kwa mpinzani wake, timu zote zilikwenda Visiwani Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi huku Simba wakiwa wa kwanza kufanya hivyo kwa kuweka Kambi yao katika Chuo kikuu cha Chukwani.

Yanga nao waliona njia rahisi ya kuwaacha midomo wazi watani wao na kuwa roho juu ni kuwafuata huko huko walikokwenda ambapo hofu sasa ilibaki kuwa ni kwa mashabiki kiasi kwamba walibaki kuangalia ni nani anayeonekana katika eneo la Bandari na kutuma ujumbe wa simu kwa wadau kuwa na Fulani ameonekana akiingia katika Boti.

Na wakati mwingine utadhani kuwa kila timu imeweka walinzi katika mageti ya kuingilia katika boti za kusafiria kuelekea Visiwani kwani kila aliyeonekana wa Simba au Yanga ujumbe ulitumwa na pia siku iliyokuwa ya mashaka kwa wanasimba ni ile alipoonekana Mwenyekiti wa Yanga Immani Madega akiingia botini kuelekea Visiwani.

Bila kujua kuwa mwenyekiti huyo pia anashughuli zake binafsi lakini bado hofu ilitanda kwa waliokuwapo Bandalini hapo walituma ujumbe kuwa inawezekana madega amekwenda kuwafuata watani wake ama kufanya lolote kuhusiana na mchezo wa leo.

Lakini pamoja na hayo yote bado mwamuzi atakuwa ni dakika 90 za mchezo, ambapo timu zote na mashabiki wa pande zote mbili kila mmoja ataingia uwanjani akiwa na furaha na majigambo lukuki na baada ya mchezo kila mmoja atatoka uwanjani hapo kwa njia yake akiwa na furaha ama majonzi.

Mchezo wa watani hawa wa jadi wa mzunguko wa kwanza katika msimu uliopita, mashabiki waliingia uwanjani huku kila mmoja akiwa na hali ya mchezo na mabango yenye maandishi ya kuwakejeli wenzao ambayo baada ya mchezo mashabiki hao wali ona mazito kila mmoja akikwepa kuyabeba na upande wa pili wakiibuka na furaha isiyo kifani jamboa ambalo pia laweza kutokea leo.

Ila ninachoweza kukudokeza ndugu msomaji ni kwamba tegemea mchezo wa amani na utulivu kwa pande zote mbili kutokana na makocha wa timu zote walivyoziandaa timu zao na kila moja ikionyesha mpira wa kufundishwa na atakayefungwa ni kweli atakuwa kafunga kihalali na pia timu zote zitakuwa zikicheza mchezo wa kujihami na mashambulizi ya kushtukiza.

Baada ya kusoma Makala haya na kuangalia vioja na matukio ya mchezo wa msimu uliopita mchezo wa mzunguko wa kwanza sasa jiandae kupata burudani kama hii live katika uwanja wa Taifa leo ama kupitia Luninga ya na matangazo ya redio, na mimi nabeba kamera yangu kuelekea uwanjani kwa ajili ya kukuandalia matukio kama haya.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.