
wenyekiti wa Klabu wa Azam, Said Mohamed (kushoto) akimkabidhi jezi na kumtambulisha mchezaji aliyejiunga na timu hiyo, Jackson Chove, wakati wa hafla fupi ya utambulisho huo iliyofanyika katika Ofisi za Klabu hiyo jijini

wenyekiti wa Klabu wa Azam, Said Mohamed (kulia) akimkabidhi jezi na kumtambulisha mchezaji aliyejiunga na timu hiyo, akitokea Yanga zote za Dar es Salaam, Mrisho Ngassa, wakati wa hafla fupi ya utambulisho huo iliyofanyika katika Ofisi za Klabu hiyo jijini.

Na Sufianimafoto, Reporter, Jijini
MSHAMBULIAJI hatari wa timu ya Taifa (Taifa Stars) na sasa Azam FC, Mrisho Ngassa, ametamba kufanya makubwa kuliko siku zilizopita ambazo watu wamekuwa wakiufahamu uwezo wake.
Hiyo inatokana na kudai kwamba ametua klabu ambayo alikuwa akiitamani muda mrefu, Azam FC, ambako alitua rasmi jana baada ya klabu yake ya zamani ya Yanga kumalizana na klabu yake ya sasa kwa dau la Sh Milioni 58.
Dau hilo pengine kwa sasa linaweza kuwa limevunja rekodi ya wachezaji wa Tanzania katika msimu huu mpya wa usajili na kuifuta rekodi ya misimu miwili iliyopita ya mchezaji Juma Kaseja, alipoihama klabu yake ya Simba na kutua kwa mahasimu wao, Yanga.
Akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya Azam leo, Ngassa alisema amefurahi kujiunga na klabu ambayo alikuwa na ndoto nayo muda mrefu, baada ya kuona kuwa ni kati ya klabu zenye uelekeo.
“Nawaahidi mashabiki wa Azam nitawafanyia makubwa mno pengine kuliko walivyokuwa wakinifahamu wakati nikiichezea klabu niliyoachana nayo, (Yanga) kwani hapa ndipo ndoto zangu zimefika,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa klabu hiyo, Said Mohamed, alisema uamuzi wao wa kumchukua Ngassa una lengo la kuhakikisha Azam inakuwa moto wa kuotea mbali na kuwa klabu mfano wa kuigwa zenye mafanikio kama ilivyo nchi za wenzetu.
Mbali ya hilo, pia uongozi huo ulimkabidhi Ngassa jezi namba 16 ya timu hiyo ambayo ni namba aliyokuwa akiivaa wakati alipokuwa akiichezea klabu yake ya zamani ya Yanga.
Katika hatua nyingine, Mohamed alisema uongozi wake umemalizana pia na mlinda mlango Jackson Chove, kuidakia timu hiyo msimu huu baada ya kulipa ada ya uhamisho kutoka timu ya JKT Ruvu aliyokuwa akiichezea ambayo alibakiza miezi sita, huku akikanusha kufahamu taarifa za mchezaji Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
“Siwezi kuzungumza juu ya Cannavaro kwa sababu suala lake halijafika mezani kwangu na kama tutakuwa tumemchukua sioni sababu za kuwaficha, tutawaambia, pengine kweli mazungumzo kati yake na sisi yanafanywa kwani ipo kamati yangu yenye majukumu hayo,” alisema.
No comments:
Post a Comment