Habari za Punde

*RAIS JAKAYA AFUNGUA MKUTANO WA TAKUKURU MWANZA



Rais Jakaya Mrisho Kikwete (KATIKATI) akiwahutubia viongozi waandamizi wa TAKUKURU wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Taasisi hiyo mjini Mwanza leo.

*TAKUKURU kujipanga kwa kazi ya kupambana na wanunuaji wa uongozi kwa kutumia sheria mpya ya matumizi ya fedha katika uchaguzi ujao

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kujipanga kwa kazi ya kupambana na wanunuaji wa uongozi kwa kutumia sheria mpya ya matumizi ya fedha katika uchaguzi.

Rais pia amezitaka Wizara za Serikali, Idara na Mashirika ya Umma kuhakikisha kuwa zinatekeleza ipasavyo Mkakati wa Taifa wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa (NACSAP) akisisitiza kuwa kama hilo likifanyika Tanzania itapata mafanikio makubwa katika kuzuia na kupambana na rushwa.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa dhamira yake ni kuhakikisha kuwa wakati anamaliza muda wake wa uongozi itakuwa imejengeka misingi imara ya utawala bora na maadili ya viongozi wa umma yenye kujikita katika sheria za nchi na baadaye kuwa utamaduni wa kudumu wa kuendesha shughuli za siasa nchini.

Rais Kikwete alikuwa anafungua Mkutano wa Mwaka wa TAKUKURU kwenye Chuo cha Benki Kuu (BOT) mjini Mwanza, leo, Alhamisi, Februari 25, 2010.

“Sheria hii inatuweka mahali pazuri kuanza mapambano na watu wanaotaka kupata uongozi kwa nguvu ya pesa. Pia inasaidia kuwabana watu wanaogeuza haki yao ya kupiga kura kuwa ni mradi au bidhaa ya kunufaika nayo kipesa kwa kuiuza,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Ole wao wahongaji, ole wao wahongwaji na ole wao wanaoomba kuhongwa.”

Rais Kikwete amesema kuwa TAKUKURU ndiyo inatazamiwa kufanya kazi ya kukazia utekelezaji wa sheria hiyo mpya. “Napenda kuwahakikishieni wana-TAKUKURU kwamba nitafanya kila liwekekanalo kuwawezesha ili muweze kufanikisha kazi ya kudhibiti rushwa katika chaguzi zetu nchini. Nataka tuanze na uchaguzu huu (wa mwaka huu)”

Kuhusu wizara, idara na mashirika ya umma kupambana na rushwa, Rais Kikwete amesema: “Swali ambalo sote hatuna budi kujiuliza na kuulizana ni je, mipango ya kila Wizara, Idara ya Serikali na Mashirika ya Umma iko wapi na kama kweli inazingatiwa na kutekelezwa. Mimi sina hakika, sijui nyie wenzangu. Naona mmerudia sifa yetu ya kuwa nguvu ya soda.”

“Napenda kutumia nafasi hii kuwakumbusha Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Idara za Serikali na Mashirika ya Umma kuhusu wajibu wao katika kuhakikisha kuwa Mkakati wa Taifa wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika maeneo yao ya uongozi uko hai na unatekelezwa kama ilivyokusudiwa.”

Rais Kikwete pia amesema kuwa kansa ya rushwa haiko katika sekta ya umma bali vile vile iko katika sekta binafsi.

“Naomba pia, hata sekta binafsi wahusishwe kwani hata na wao wanahusika katika vitendo vya rushwa. Wapo maofisa na watendaji katika makampuni binafsi wanaojihusisha na vitendo vya kutoa, kudai, na kupokea rushwa. Wanafanya hivyo katika ajira, kutafuta masoko na kutafuta zabuni. Bahati mbaya sana hata waandishi wa habari nao hawako salama katika kadhia hii. Hivyo, rushwa iko kila mahali, sote tuhusike na kuhusishwa katika mapambano hayo.”

Rais Kikwete ameisifu TAKUKURU kwa kazi nzuri katika kupambana na rushwa na kusisitiza kuwa la msingi ni kwamba taasisi hiyo isimwonee haya mtu ambaye ni mhalifu lakini vile vile isimwonee mtu ambaye hana makosa. “Tendeni haki kwa kuzingatia Katiba, Sheria na Kanuni. Matunda ya kazi yetu yataonekana.”

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.