Habari za Punde

MEKEZAJI WA SUN BIOFUEL NCHINI APONGEZWA



























Meneja Mkuu wa Kampuni ya Sun Biofuels , Peter Auge. akitoa maelezo mafupi kwa Mkuu wa wilaya ya Kisarawe, Bi Hanifa Karamagi.














Meneja Mkuu wa Kampuni ya Sun Biofuels , Peter Auge. akitoa maelezo mafupi kwa Mkuu wa wilaya ya Kisarawe, Bi Hanifa Karamagi.













Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Bibi Hanifa Karamagi, (kulia) akizungumza na wafanyakazi wa mradi wa zao la Jatropha wilayani humo wakati wa zara ya kukagua mradi wa zao la Mibono na Jatropha mwishoni mwa wiki. Mradi huo unaomilikiwa na mwekezaji kutoka nchini Uingereza, Peter Auge chini ya Kampuni ya Sun Biofuels kwa lengo la kuzalisha nishati ya mafuta ya dizeli.




Na Mwandishi Maaalum.

Serikali wilayani Kisarawe, imempongeza mwekezaji wa zao la Jatropha wilayani humo, kampuni ya Sun Biofuel ya Uingereza, kwa kazi nzuri inayofanya wilayani Kisarawe na wakati huo huo kuwahakikishia wananchi wa Vijiji 11 wilayani Kisarawe ambao ardhi yao imemilikishwa kwa mwekezaji huyo kulipwa fidia zao baada ya uchambuzi yakinifu.
Pongezi hizo zimetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Bibi Hanifa Karamagi, mara baada ya kufanya ziara ya kukagua mradi huo, unaomilikiwa na mwekezaji kutoka nchini Uingereza, kampuni ya Sun Biofuels, ambayo inafanya mradi wa kilimo cha zao la Jatropha, au jina maarufu la Mibono Kaburi, kwa lengo la kuzalisha mafuta ya dizeli.
Bibi Karamagi ametoa pongezi kwa mwekezaji huyo kwa kutoa ajira rasmi zaidi ya 400 kwa wanavijiji wa vijiji vinavyozunguka mradi huo ikiwa ni pamoja na kuwalipia mafao NSSF, na kusema ajira hizo zitaboresha maisha ya wanavijiji hao, na akawasisitiza wanavijiji hao, wasibweteke na fedha za mishahara kwa kufanyia starehe, kulewa na kuongeza idadi ya wanawake, bali wazitumie fedha hizo kuboresha maisha yao na kujiletea maendeleo, ikiwemo kuendeleza kilimo cha mazao ya chakula huko vijijini kwao.
Bibi Karamagi amesema, kampuni hiyo ya uwekezaji toka nchini Uingereza, ilifuata sheria, taratibu na kanuni zote za uwekezaji na umilikaji ardhi ya vijiji kwa mujibu ya Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba 5 ya Mwaka 1999, ikiwemo kulipa fidia stahiki kwa vijiji husika, hivyo serikali inafanya uchambuzi yakinifu kubaini kama kuna wanavijiji wowote ambao hawakupata malipo ya fidia zao kwa namna moja ama nyingine.

Katika ziara hiyo, Mkuu huyo wa wilaya aliyekuwa amefuatana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Kisarawe, amejionea takriban hekari 1000 ambazo zimeshalimwa na kupandwa zao hilo, ikiwemo kushuhudia baadhi ya micheche ambayo tayari imeshazaa matunda hayo ambayo mbegu zake hutumika kuzalisha mafuta ya dizeli ambayo ni rafiki wa mazingira.

Akimkaribisha mkuu wa wilaya, Meneja wa Kampuni hiyo ya Sun Biofuel nchini Tanzania, Peter Auge, amesema, kati ya ekari 8200 ambazo kampuni yake imemilikishwa, ni 6,000 tuu ndizo zitatumika kwa kwa kilimo cha mibono, na eneo lililobakia litatumika kama eneo la hifadhi ya misitu asilia. Pia kampuni hiyo, itaongeza ajira toka 400 zilizopo sasa mpaka 1500 katika kipindi cha miaka mine ijayo.
Vijiji vya Mtamba, Muhaga, Marumbo, Paraka, Kidugalo, Kului, Mtakayo, Vilabwa, Mitengwe, Mzenga ‘A’ na Chakaye ndivyo wafaidika wakuu wa mradi huo, ambapo licha ya wanavijiji hao kupa ajira za moja kwa moja, kwenye mradi huo, mwekezaji huyo wa Sun Biofuel, atawajibika kuboresha huduma za jamii ukiwemo upatikanaji wa maji safi na salama, na kuchangia huduma mbalimbali za maendeleo ikiwemo miradi ya afya na elimu.
Kampuni ya Sun Biofuel (T) Ltd, inamilikiwa kwa ubia kati ya Watanzania na Waingereza ambapo imejikita katika kilimo cha zao hilo la Jatropha kwa jina maarufu la Mibono Kaburi ambalo hustawi kwenye ardhi kame na isiofaa kwa kilimo cha mazao ya chakula.
Tanzania ina maeneo mengi yasiyofaa kwa kilimo, hivyo kuishia kukaa bure, hali inayopelekea kilimo cha zao hili la mibono, kuonekana kama mkombozi wa matumizi sahihi ya ardhi iliyokuwa inakaa bure, na wakati huo huo kutoa ajira kwa maelfu ya waTanzania.



No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.