Habari za Punde

*NAKAAYA SUMARI AHAMIA KWENYE SIASA, AJIUNGA CHADEMA


Na Eliya Mbonea,Arusha

MWANAMUZI wa miondoko ya kizazi kipya wa ‘Bongo Fleva’ Nakaaya Sumari. ametangaza rasmi kujiunga na siasa katika Kambi ya upinzani na tayari amekabidhiwa kadi namba 0227706 ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Akizungumza na Sufianimafoto Reporter jijini Arusha leo, Nakaaya alisema, hakusukumwa wala kushawishiwa na mtu yeyote kujiunga na masuala ya siasa
hususani za kambi ya upizani bali aliamua mwenyewe kuchukua hatua hiyo muhimu ili kuleta mabadiliko ndani ya jamii ya Watanzania.
Nakaaya ambaye hivi karibuni alipata kutamba na kibao chake cha ni ‘Mr Politician’ kilichokuwa kikizungumzia zaidi mambo ya Siasa ambayo hufanywa na baadhi ya wagombea ambao huomba kura kwa kubembeleza lakini baada ya kupata hushindwa kufikisha kusudi na matatizo yanayowakabili wananchi katika sehemu husika badala yake hulenga zaidi maslahi binafsi.
Akizungumza kwa kujiamini zaidi alisema sababu zilizomsukuma kujiunga na CHADEMA, kuwa ni pamoja aina ya maisha ya ambayo Watanzania wengi wamekuwa wakiishi bila kujua hatima ya maisha yao kwa kukosa huduma nyingi muhimu.
Aidha alisema katika mazingira kama hayo Serikali imekuwa ikiingiza fedha nyingi hususani katika Sekta za Afya lakini miaka nenda rudi bado akina mama na wajawazito wameendelea kufariki dunia kwa kujifungua bila kuwa na vifaa muhimu huku wengine wakilala katika kitanda kimoja wanawake sita au wane katika wodi za wazazi.
“Hii ni fedheha kwetu kama Watanzania hususani akina mama, inakuwaje leo tangu Uhuru tuendelee kulala chini baada ya kujifungua ndani ya hospitali zetu, viongozi wa serikali wamekuwa wakiwadharau akina mama ndiyo tasfiri yake,” alisema Nakaaya.
Akitoa sababu nyingine, mwanamuzi huyo ambaye hajatoa nyimbo nyingine alibainisha kwamba, hivi sasa shilingi ya Tanzania imeendelea kuporomoka ikilinganishwa na baadhi ya fedha za nchi nyingine ambazo tangu zipate uhuru wao zimeendelea kukumbwa na migogoro ya vita vya wenyewe kwa wenyewe lakini bado fedha zao zimeendelea kuimarika zaidi kuliko shilingi ya Tanzania.
“Hii ilikuwa ni ndoto yangu ya muda mrefu lakini pia nimekuwa nikikerwa na umasikini wa Watanzania wenzangu ilhali bado tumejaliwa kuwa na rasilimali nyingi kuliko hata za nchi zinazotuzunguka,” alisema Nakaaya mbele ya viongozi wa CHADEMA Mkoa wa Arusha.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Vijana CHADEMA mkoani Arusha, Exaud Mamuya akizungumzia hatua hiyo ya Nakaaya na kumpongeza kwa kuamua kujiunga na siasa kwa lengo la kuwatetea kina mama wenzake kupitia CHADEMA.
http://www.sufianimafoto.blogspot.com/

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.