Habari za Punde

*SOKO LA MJI MDOGO WA SIRARI LAKITHIRI KWA UCHAFU

Lundo la takataka likiwa limetapakaa nje ya Soko la mji mdogo wa Sirari wilayani Tarime Mkoani Mara bila kuzolewa kwa wakati, jambo linaloweza kusababisha magonjwa ya mlipuko wakati wowote, huku Nguruwe wakijivinjari katika taka hizo kusaka msosi nje ya soko hilo.

Na Christopher Gamaina, Sirari Tarime
WAKAZI mji mdogo wa Sirari wilayani Tarime, wanakabiliwa na hatari ya kukumbwa na magonjwa ya mlipuko wakati wowote, ikiwa mamlaka husika hazitachukua hatua ya kuwaondolea haraka rundo la uchafu wa kila aina katika soko na kituo cha daladala mjini hapo.
Wakizungumza na wanahabari mjini Sirari jana, wakazi wa mji huo waliushutumu uongozi wa idara ya afya katika Wilaya ya Tarime kuruhusu eneo hilo kugeuzwa jalala la uchafu wa kila aina, hali inayosababisha kero na bughudha kubwa kwa watumiaji wa eneo hilo.
Waandishi wa habari walishuhudia rundo kuwa la uchafu wa aina mbalimbali yakiwamo machungwa yaliyooza, mifuko ya plastiki yenye vinyesi vya binadamu na mizoga ya mbwa na paka, huku makundi ya nguruwe yakivijari ndani jalala hilo.
Aidha, wanahabari walishuhudia makundi ya inzi wakiruka kutoka jalalani hapo na kwenda kutua ndani ya migahawa ya chakula na vinywaji vilivyo jirani, hali inayohatarisha afya za watu wanakwenda kupata huduma kwenye migahawa hiyo.
Kwa mujibu wa wananchi hao, jalala hilo halijashughulikiwa kwa namna yoyote kwa zaidi ya miezi minne sasa na kwamba baadhi ya watoto wamekuwa wakienda kuokota na kula matunda mabovu yaliyooza ndani ya jalala hilo.
“Kwa kweli wakazi wa Sirari tunahofu ya kukumbwa na magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu na kuhara damu kutokana na jalala hili, kini uchafuzi huu wa mazingira unatuabisha kwa majirani zetu Wakenya wanaokuja kujinunulia mahitaji katika soko hili,” alilalamika Nyabilonkoni Marwa.
Kaimu Ofisa Afya wa Wilaya ya Tarime, Joseph Marwa, alipoulizwa alisema ofisi yake iko mbioni kuanza kutekeleza zoezi la kuhamisha uchafu huo na kuweka mazingira ya eneo hilo katika hali ya usafi.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.