Habari za Punde

*TUME YA HAKI ZA BINADAMU YAWASILISHA RIPOTI YAKE KWA VYOMBO VYA UTEKELEZAJI WA HAKI

Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi

Tume ya Haki za Binadami nchini imewasilisha ripoti yake ya uchunguzi wa malalamiko dhidi ya vyombo vya utendaji na kuwaagiza Viongozi wa Serikali waliopo madarakani kuhakikisha wanaweka misingi bora inayozingatia haki za binadamu.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Haki za binadamu nchini Jaji Kiongozi Mstaafu Amiri Manento, wakati wa mkutano wa kuwasiliasha taarifa ya uchunguzi wa mambo ya ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa na Tume hiyo katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
Jaji Manento amesema kuwa kama kila kiongozi na mtumishi wa umma wataweka misingi imara ya kulinda haki za binadamu kwa lengo la kuliwezesha taifa na vizazi vijavyo viwe na maadili mema.
Katika mkutano huo uliohudhuliwa na Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Wawakilishi kutoka ofisi ya Rais Utawala Bora, Jaji Manento amesema kuwa kila mtu anastahili heshima na kuthaminiwa utu wake.
Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti na Nyaraka ya Tume ya Haki za Binadamu nchini Bi. Epiphania Mfundo, amesema kuwa chimbuko la utafiti huo unatokana na kuongezeka kwa vitendo vya kikatili na mateso kwa raia wasiokuwa na hatia na wale wanaotuhumiwa kutenda makosa.
Amesema kuwa ukatili unaozungumzwa katika zoezi hilo ni ule unaweza kuwafanywa na watendaji wa vyombo vya kutekeleza sheria katika kutimiza wajibu wao wa kuhakikisha kuwa sheria na taratibu za nchi zinafuatwa.
Bi Mfundo amevitaja baadhi ya vyombo vilivyolalamikiwa na wananchi wakati wa utafiti huo kuwa ni Polisi, Mgambo, Sungusungu, Uhamiaji, Waendesha mashitaka, Mahakama, Watendaji wa Mikoa, Watendaji wa Wilaya, Watendaji wa Tarafa, Kata, na Vijiji.
Wengine waliolalamikiwa ni Watendaji wa TANESCO, TRA, Hospitali, Ardhi, Maliasili, Vyombo vya Habari, Elimu na Watendaji wa Tume ya Utumishi wa Umma.
Ameyataja baadhi ya mambo yanayolalamikiwa na wananchi waliowengi kuwa ni pamoja na vipigo, unyanyasaji na kubambikiza kesi kunakofanywa na baadhi ya Askari Polisi, Magereza, Mgambo, Maliasili, Takukuru na TRA.
Vitendo vingine vilivyolalamikiwa ni upendeleo, kuandika habari za uchonganishi, kunyima ama kuchelewesha utoaji wa nakala ya hukumu, kutozingatia maadili ya utumishi wa umma vinavyofanywa na watumishi wa idara za Mahakama, Uhamiaji, Afya,Watendaji wa Mikoa, Wilaya, Tarafa na vijiji.
Wengine waliolalamikiwa katika taarifa hiyo ni baadhi ya Watendaji wa Shirika la Umeme nchini TANESCO ambao wanalalamikiwa kwa kubambikiza bili tofauti na matumizi halisi ya mteja, kupeleka huduma za kuunganisha umeme kwa upendeleo ama kukata umeme pasipo sababu za msingi mambo ambayo yanapelekea kushamiri kwa vitendo vya rushwa.
Mambo mengine yaliyomo katika ripoti hiyo ni vitendo vya ukatili bila ya kujali sababu ambavyo mara nyingi vimekuwa ni kichocheo cha rushwa na ukiukwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora.
Hata hivyo Bi. Mfundo amesema kuwa wakati wa utafiti huo, wamebaini kuwa mpango na mkakati wa elimu ya Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vitendo vya kikatili vilivyokuwa vikifanywa na askari wa Sungusungu katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Tume ya Haki hiyo Bi. Mary Masai, amesema kuwa vitendo vingi vya unyanyasaji, vimekuwa vikifanywa na watu binafsi bila shinikizo la Taasisi husika kwa lengo la kujipatia rushwa kwani amesema kuwa uhusiano kati ya rushwa na ukatili ni mambo yaliyojitokeza wakati wa utafiti wa taarifa hiyo.
Mambo mengine yaliyotajwa katika ripoti hiyo ni kuongezeka kwa vitendo vya kikatili vinavyofanywa na wananchi kwa kivuli cha chuki na hasira kali kwa watuhumiwa wa makosa ya kijinai kama vile kuwachoma moto ama kuwapiga hadi kuwaua watenda makosa.
Wakichangia hoje kwenye taarifa hiyo Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali Saidi Mwema na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Bw. Bampikya Willibard, wamesema baadhi ya vitendo vinavyotokea nchini vinatokana na kuporomoka kwa maadili miongoni mwa watanzania.
IGP Mwema, amesema kuwa wizi wa mitihani ama kula njama na kumuonyesha mwanafunzi matokeo ya mitihani ni kukosa uaminifu na kuporomoka kwa maadili.
Kwa upande wake Bw. Willibard, amesema haki za binadamu ziwajali pia Askari Polisi ambao mara nyingi wamekuwa wakipatwa na maafa wakiwa kazi lakini hakuna chombo kinachoweza kuwasemea lakini Haki za Binadamu zinawatetea wahalifu kama wakifanyiwa vibaya na Polisi.
Mkutano huo umehudhuriwa na Viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama hapa nchini wakiongozwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali Saidi Mwema.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.